Home Kitaifa NHIF YAIMARISHA UWEZO WA KIFEDHA, MAPATO YAPANDA ASILIMIA 10.3

NHIF YAIMARISHA UWEZO WA KIFEDHA, MAPATO YAPANDA ASILIMIA 10.3

Celebrating 25 Years of NHIF

DAR ES SALAAM

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeimarisha hali yake ya kifedha, kupanua mtandao wa vituo vya huduma za afya na kuongeza ufanisi wa ulipaji wa madai, ikiwa ni sehemu ya mafanikio yake katika kipindi cha miaka 25 tangu kuanzishwa kwake.

FAHARI AFYA

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dkt. Irene Isaka, amesema mafanikio hayo yametokana na kuboresha usimamizi wa rasilimali, kudhibiti matumizi na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wanachama.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Novemba 6, 2026, Dkt. Isaka amesema mapato ya Mfuko yameongezeka kwa asilimia 10.3, huku matumizi yakipungua kwa asilimia 10, na kushusha uwiano wa gharama za matibabu dhidi ya mapato kutoka asilimia 87 hadi asilimia 71, karibu na kiwango cha asilimia 70 kinachotajwa kimataifa kwa uimara wa mifuko ya bima ya afya.

Amesema muda wa wastani wa kulipa madai ya watoa huduma umepungua kutoka siku 120 hadi 50, chini ya ukomo wa siku 60 unaotajwa kisheria. Aidha, wanachama wakuu wameongezeka kwa asilimia 17, wategemezi kwa asilimia 6.2, huku mtandao wa vituo vinavyoshirikiana na NHIF ukifikia zaidi ya 10,300.

Katika kuadhimisha miaka 25, NHIF imepanga maonesho ya siku saba katika viwanja vya Kinangari, Dodoma, kuanzia Novemba 23 hadi 29, 2026, pamoja na marathon inayotarajiwa kushirikisha zaidi ya watu 10,000.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, ameipongeza NHIF kwa kutambua mchango wa wanahabari katika kuelimisha umma na kuhamasisha wananchi kujiunga na bima ya afya.

Balile amesema nafasi 100 za bima ya afya zilizotolewa kwa wanahabari ni fursa muhimu, akishauri ziwafikie zaidi waandishi na wahariri wanaofanya kazi bila kuwa na bima. Ameeleza kuwa TEF itashirikiana na NHIF kuweka utaratibu wa kuwatambua wanahabari wenye uhitaji huo.

“Tutaendelea kuhamasisha na kuongeza nguvu ili kuhakikisha Watanzania wanaielewa dhana ya bima ya afya na umuhimu wake,” amesema Balile, akisisitiza kuwa TEF itaendelea kushirikiana na NHIF katika kuelimisha umma na kuunga mkono maadhimisho ya miaka 25 ya Mfuko huo.

Naye Mratibu wa Elimu kuhusu Bima ya Afya kwa Wote kutoka Wizara ya Afya, Said Makora, amesema Serikali inaendelea kuongeza watumishi wa afya kujiandaa na mahitaji yatakayoongezeka kutokana na utekelezaji wa mpango wa bima ya afya kwa wote. Amesema kati ya ajira 5,000 zilizotolewa katika sekta hiyo, watumishi 808 wamepelekwa katika ngazi ya huduma za afya ya msingi, zikiwemo hospitali na vituo vya afya.

Hata hivyo, Makora amesema bado kuna upungufu wa watumishi wa afya, hivyo Serikali inaendelea kushirikiana na wadau na kutumia mikakati mbalimbali kuongeza wataalamu na kuwapeleka katika maeneo yenye uhitaji.

Ameeleza kuwa maandalizi hayo hayahusu kuongeza idadi ya watumishi pekee, bali pia kuhakikisha kunakuwa na wataalamu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya huduma mbalimbali za afya.

“Sio idadi tu ya watumishi, bali pia tunahitaji wataalamu wanaokidhi mahitaji katika maeneo yote muhimu ya huduma za afya,” amesema Makora, akitaja huduma za mama na mtoto, saratani na maeneo mengine muhimu ya matibabu kuwa miongoni mwa yanayohitaji wataalamu.

Maadhimisho ya miaka 25 ya NHIF yanafanyika wakati Mfuko ukiendelea kuboresha usimamizi wa fedha, mifumo ya utoaji huduma na ushirikiano na vituo vya afya, kwa lengo la kuongeza uwezo wa kuwahudumia wanachama na kuchangia upatikanaji wa huduma bora za afya kwa Watanzania.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!