
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amewasili Songea mkoani Ruvuma leo tarehe 26 Februari 2026, kwa ajili ya kushiriki maadhimisho ya kilele cha Tamasha la Kumbukumbu ya Miaka 120 ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji.
Makamu wa Rais anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha tamasha hilo litakalofanyika tarehe 27 Februari 2026 katika Viwanja vya Makumbusho ya Majimaji, Songea.

Katika Uwanja wa Ndege wa Songea, Mhe. Nchimbi amepokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Hamad Chande, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho, pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, taasisi, dini, vyama vya siasa, wananchi wa Ruvuma na machifu wa kabila la Wangoni kutoka Afrika Kusini, Malawi na Tanzania.
Tamasha la Kumbukumbu ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji hufanyika mwezi Februari kila mwaka likiwa na lengo la kuwakumbuka mashujaa wa Tanzania waliopigana Vita vya Majimaji kupinga ukoloni. Tamasha hilo la kihistoria linatarajiwa kuhusisha shughuli mbalimbali za kitamaduni, maonyesho ya historia na burudani zinazoakisi urithi na utamaduni wa wananchi wa kusini mwa Tanzania.








