Home Kitaifa NAIBU WAZIRI KATAMBI APONGEZA MFUMO WA KUINGIA MIKATABA YA UTENDAJI KAZI NA...

NAIBU WAZIRI KATAMBI APONGEZA MFUMO WA KUINGIA MIKATABA YA UTENDAJI KAZI NA TAASISI ZA UMMA

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amepongeza Mfumo wa kuingia Mikataba ya Utendaji Kazi na Taasisi za Umma ambao unaainisha malengo yatakayo tekelezwa na Taasisi za Umma katika kipindi cha mwaka mmoja.

Ameyasema hayo hii leo Agosti 14, 2022 Jijini Arusha wakati wa kikao kazi cha menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu cha kufanya tathmini ya utendaji kazi wa kwa mwaka 2021/22 na kuweka malengo, na kusaini mikataba ya Utendaji Kazi kwa Mwaka 2022/23.

“Mfumo huu una faida nyingi ikiwa ni pamoja na kuongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa Sera, Mikakati na vipaumbele vya Taasisi za umma na vya kitaifa”

Pamoja na hayo Mhe. Katambi ameisisitiza menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu kufanya kazi kwa bidii na kuwa wabunifu katika maeneo yao ya kazi ili kuongeza tija na ufanisi katika kazi tunazozifanya;

Aidha, amehimiza mshikamano na kufanya kazi kama timu kwa kuwa, Ofisi hiyo ndiyo Kioo na Kiongozi kwa Wizara nyingine, hivyo amewataka kuweka usimamizi madhubuti katika Programu, Miradi na kazi zote ambazo zinasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Prof. Jamal Katundu ameeleza kuwa mikataba hiyo ya utendaji kazi itasaidia ofisi hiyo na taasisi zilizopo chini yake kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kutekeleza kwa ufanisi maelekezo wanayopatiwa na Viongozi na hatimaye kuleta maendeleo kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Kikao kazi hicho kilishirikisha pia Wakuu wa Taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo ikiwemo Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA).

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!