Home Kitaifa MKIFUATA USHINDANI KATIKA SOKO MTAZALISHA BIDHAA BORA- JAFFO

MKIFUATA USHINDANI KATIKA SOKO MTAZALISHA BIDHAA BORA- JAFFO

Waziri wa Viwanda na Biashara wa Tanzania Dkt. Selemani Jafo amewataka wawezekaji wazawa na wafanyabiashara kuhakikisha wanatumia fursa ya masoko mbalimbali ya ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora na kwa kuzingatia sera na taratibu za ushindani.

Waziri Jafo ameyasema hayo siku ya Alhamisi Desemba 05, 2024 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ushindani Duniani ambayo kwa Tanzania yamefanyika katika hoteli ya Golden Tulip mkoani Dar es Salaam chini ya uratibu wa Tume ya Ushindani (FCC).

Waziri Jafo amesema fursa za masoko ya Ulaya, China na AGOA (Mpango wa Ukuaji na Fursa kwa Afrika unaowezesha mataifa ya Afrika kusafirisha bidhaa Marekani bila ushuru) zinaweza kutumika vyema kwa kuwa na kiwango kikubwa cha bidhaa zenye ubora mkubwa ambazo pasina ushindani haziwezi kupatikana.

Ukiachia soko la ndani, tuna upana mkubwa wa soko la Afrika Mashariki, halikadhalika tuna soko la SADC na vilevile tuna soko huru la Afrika. Kupitia soko huru la Afrika, Watanzania wanaweza kufanya biashara na nchi zaidi ya 50. Hii ni fursa kubwa kwa Watanzania, lakini huko lazima tuelewe kwamba lazima tuzalishe bidhaa zilizokuwa bora ziweze kushindana na za wenzetu, bila kufanya hivyo hatuwezi kupata fursa za kufanya vizuri biashara hii”, ameeleza Jafo.

Aidha amesema kuwa miongoni mwa mambo ya kufanya ili kuleta ushindani ni kuongeza uelewa na kujadili biashara ya ushindani kwa kuzalisha bidhaa bora za kushindana kwenye soko.

Katika soko la AGOA tumepata fursa ya kuuza zaidi ya bidhaa 6500, lakini mauzo yetu yamekuwa madogo, hayaakisi uhalisia wa bidhaa ambazo nchi inazo“, amesisitiza Jafo.

Aidha amesema nchi imeendelea kuweka mazingira rafiki na fursa mbalimbali za uwekezaji ikiwamo mabadiliko ya sera, na uwepo wa taasisi za serikali ambazo zimeendelea kuboresha utendaji wake kama FCC, na TIC.

Katika kuchagiza zaidi hilo, ametoa maelekezo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara kuangalia kama kuna kanuni au sheria yoyote ambayo inawakwamisha wafanyabiashara kufanya biashara kwa kushindana inaweza kufanyiwa mchakato wa kuboreshwa.

Halikadhalika amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa FCC William Erio kuharakisha mchakato wa kampuni zinazotaka kuunganishwa (Mergers) ili kuchochea zaidi uchumi, na kuchagiza utoaji wa ajira hasa kwa vijana wa Tanzania.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Ushindani (FCT), Jaji Salma Maghimbi amesema maadhimisho ya Siku ya Ushindani ni muhimu katika kujadili mambo muhimu yanayolinda uchumi ili kuwa na uchumi wenye mizania na haki sawa.

Amesema kwamba wao kama FCT wanatambua kuwa ushindani ni kiungo maalumu katika maendeleo ya nchi, akieleza kuwa kunapokuwa na ushindani wa haki, kunakuwepo na uvumbuzi mpya na utoaji wa huduma zenye ufanisi.

Aidha amesema ushindani usipokuwepo kutakuwa na watu wanaodhibiti soko, wanaokandamiza wengine kwa kuongeza bei kwa walaji, lakini pia kuzuia biashara ndogo kuingia sokoni.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa FCC Dkt. Aggrey Mlimuka ameeleza kuwa FCC ina dhamana ya kushajihisha ushindani wa haki katika biashara kwa kuakisi Kaulimbiu ya maadhimisho hayo isemayo ‘Sera ya Ushindani na Kudhibiti Kukosekana kwa Usawa katika Uchumi’.

FCC ina jukumu la kuhakikisha kuwa soko linaendelea kubaki shindani ili walaji waweze kunufaika na uwepo wa ushindani katika soko, na hivyo kuchochea ukuaji endelevu na mjumuisho katika uchumi wa taifa letu“, ameeleza Mlimuka.

Amesema FCC imesema imejitahdi kuboresha utendaji wake ili kuboresha misingi ya ushindani katika soko na ipo mbioni kukamilisha taratibu za kupatiwa cheti cha ubora wa huduma cha
Kiwango cha Ubora wa Kimataifa (ISO 9001:2015) ili iweze kuwatumikia vyema Watanzania.

Maadhimisho hayo yameambatana na kongamano lililowakutanisha wafanyabiashara, wawekezaji, viongozi wa taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi, wataalamu wa uchumi pamoja na wanafunzi wa vyuo mbalimbali ambao wamejadili masuala mtambuka yanayohusu ushindani katika biashara.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!