Home Biashara MHE. KIGAHE AIAGIZA BODI YA USIMAMIZI WA STAKABADHI ZA GHALA (WRRB) KUHAKIKISHA...

MHE. KIGAHE AIAGIZA BODI YA USIMAMIZI WA STAKABADHI ZA GHALA (WRRB) KUHAKIKISHA WANAJENGA MAGHALA YA KISASA

Naibu Waziri Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe ameiagiza Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) kuhakikisha inajenga maghala ya kisasa ili wakulima waweze kuhifadhi na kuongeza ubora wa mazao yao ambayo yatapata bei nzuri.

Ameyasema hayo Leo tarehe 30 Juni, 2022 katika uzinduzi wa siku ya stakabadhi za ghala katika Maadhimisho ya siku ya Ushirika Duniani yanayofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nane nane Mkoani Tabora.

Mhe. Kigahe amesema kuwa Kuna umuhimu mkubwa wa wakulima kuyahifadhi mazao yao sehemu salama ambayo yatakuwa na ubora na Bei nzuri.

Mhe. Kigahe ameongeza kuwa Maghala ni muhimu na ndio maana Serikali inaona umuhimu wa kuwasaidia wakulima katika kuhifadhi mazao yao kutokana na changamoto wanazopata za kushindwa kuhifadhi mazao Mahali salama na pa uhakika.

Mhe. Kigahe Amebainisha kuwa Serikali inasisitiza umuhimu wa mfumo wa stakabadhi ghalani ambao una manufaa makubwa kama mkulima kuuza mazao yake kwa Bei ya soko, kuhifadhi mazao sehemu salama na uhakika wa takwimu.

“Dunia kwa Sasa ina ushindani wa soko, hivyo ni muhimu kuwa na mfumo unaoeleweka kama wa stakabadhi ghalani ambao pia unatoa uhakika wa chakula” Amesema Mhe. Kigahe.

Mhe. Kigahe ameeleza manufaa ya mfumo wa stakabadhi ghalani na kueleza faida wanazopata wakulima ambapo amesema kuwa ongezeko la bei ya mazao tangu kuanzishwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kuwa ni asilimia 257 kwa zao la Choroko, asilimia 250 kwa zao la Kakao na asilimia 168 kwa zao la korosho.

Kwa upande wa changamoto Mhe. Kigahe ameeleza kuwa bado Kuna uelewa finyu kuhusu manufaa ya mfumo wa stakabadhi ghalani na uhaba wa maghala na ndio maana ameagiza ujenzi wa maghala kuwasaidia wakulima na elimu kuendelea kutolewa kwa wananchi na wakulima kuhusu manufaa ya mfumo huo.

Mrajis wa Vyama vya Ushirika Nchini, Dkt. Benson Ndiege, amewasisitiza wakulima kuchangamkia mfumo wa stakabadhi ghalani ambao Bei inakuwa nzuri kwa vile mazao yanakuwa Bora.

Amewataka watumishi katika sekta ya Ushirika kutofanya kazi kwa njia ya ujanja ujanja Bali kwa uaminifu ili Ushirika uwe na manufaa kwa wanaushirika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!