Home Kitaifa MHE. KHAMIS HAMZA KHAMIS AMEWATAKA WANANCHI KUACHA KUVAMIA NA KUHARIBU VYANZO VYA...

MHE. KHAMIS HAMZA KHAMIS AMEWATAKA WANANCHI KUACHA KUVAMIA NA KUHARIBU VYANZO VYA MAJI.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amewataka wananchi kuacha kuvamia na kuharibu vyanzo vya maji.

Pia amekemea tabia ya baadhi watu kufanya makazi katika maeneo yasiyostahili yakiwemo kwenye vyanzo vya maji hali inayochangia uharibifu wa mazingira.

Mhe. Khamis alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa hadhara na wananchi wa eneo la Ubaruku Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya wakati wa ziara ya Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta.

Alionesha kutofurahishwa na uharibifu wa vyanzo hivyo mara baada ya kutembelea eneo la Mto Ruaha na Mnazi katika kijiji cha Mwanavala vilivyopo ndani ya hifadhi.

Naibu waziri huyo alionya tabia ya baadhi ya wananchi kufanya shughuli za kibinadamu zikiwemo kuingiza mifugo na kufanya makazi katika maeneo yenye vyanzo vya maji.

Tumeshuhudia vyanzo vya maji vimeharibiwa sana, maji yale ndio yanayotusababishia sisi kuishi, maji yale ndio yanayosukuma umeme ukapatikana, maji yale ndio viumbe hai wanasurvive sasa tumeliona lile bonde kule hali ni mbaya, tukikaa kimya tutaelekea pabaya,alitahadharisha.

Aidha, Mhe. Khamis alisema hajafurahishwa na tabia ya ukataji miti holela inayofanyika katika baadhi ya maeneo hapa nchini hali inayosababisha uharibifu wa mazingira.

Alisema endapo wananchi wataendelea na tabia ya ukataji miti mvua itakuwa ni ndoto hali itakayosababisha ukame ambao ni chanzo cha ukosefu wa maji kwa ajili ya mifugo na shughuli za kilimo.

Ndugu zangu naomba niwaambie mazingira ndiyo kila kitu tusipoyatunza mazingira hayatatutunza, cha msingi nataka nitoe wito Tanzania nzima watu wapande miti, watunze vyanzo vya maji, watunze mazingira, watu waheshimu sheria na taratibu zote zinazohusiana na masuala ya mazingira,alisema.

Tayari Kamati hiyo imeshatembelea mikoa mbalimbali na inaendelea na ziara yake kwenye mikoa mingine ya Iringa, Njombe na Ruvuma.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!