
Wakulima wa zao la choroko wilayani Bunda mkoani Mara wameishukuru serikali kuja na mpango wa ununuzi wa mazao mchanganyiko kwa mfumo wa stakabadhi za ghala kwani itasaidia kudhibiti mazao yao kununuliwa kwa njia ya ulanguzi.
Kauli hiyo wanaitoa mara baada ya kupata mafunzo ya muongozo kuelekea msimu wa ununuzi wa zao la choroko kwa mkoa wa Mara, na hapa wanasema stakabadhi za ghala zimerejesha heshima kwa wakulima kwani kipindi cha nyuma walikuwa wakipitia manyanyaso yasiyostahili ikiwemo kuuza mazao yao katika njia zisizo sahihi kwa mawakala hali iliyokuwa ikipelekea wakichukia kilimo lakini kwa sasa hali ni shwari.

Kwa upande wa mwenyekiti wa chama kikuu cha Pamba Cooperative Union Ndaro Lubunda aliwataka wakulima hao kuepukana na tabia za utoroshaji wa mazao kwani serikali imewawekezea mazingira bora katika eneo hilo ili kuhakikisha wananufaika na wanachokilima.
Aidha, Mrajisi msaidizi wa vyama vya Ushirika mkoa wa Mara Lukasi Kondere alisema katika ununuzi wa choroko mwaka huu wanatarajia kununua kilo milioni huku akiwataka wakulima kuzingatia ubora wa mazao ikiwemo kuepuka uchafu kwenye mazao ambayo yataingizwa mnadani.








