Home Biashara MAVUNDE: TUMIENI TAKWIMU KUBORESHA KILIMO Na:Saidi Ibada, Singida

MAVUNDE: TUMIENI TAKWIMU KUBORESHA KILIMO Na:Saidi Ibada, Singida

Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde amezitaka taasisi zinazojishughulisha na kilimo kutumia takwimu kutoka Shirika la Takwimu nchini (NBS) ili kuboresha sera kwa lengo la kuimarisha uhimilivu katika sekta ya Kilimo ili kukidhi mahitaji ya Taifa na soko la Dunia kiujumla.

Ameyazungumza hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya Takwimu Afrika ambayo kitaifa yameadhimishwa Mkoani Singida yakiongozwa na kauli mbiu isemayo “Kuimarisha Mifumo ya Kitakwimu kwa kutumia Njia za Kisasa katika uzalishaji na Matumizi ya Takwimu za Kilimo ili kuboresha Sera kwa lengo la kuimarisha Uhimilivu Katika Kilimo, Lishe na Usalama wa Chakula Afrika”.

Naibu Waziri Mavunde amesema ipo haja kwa taasisi, mashirika pamoja na watu binafsi kijikita katika kilimo cha kisasa kwa minajili ya kuinua na kuimarisha mifumo ya kilimo hapa Nchini.

“Sasa hivi tunaendelea na zoezi la usajili wa wakulima ili tujue idadi yao na aina ya mazao wanayolima. Ofisi ya Takwimu wametoa taarifa zao ni wajibu wetu sisi wadau kuzitumia hizo takwimu kwa lengo la kuimarisha kilimo. Natoa rai kwa wataalamu wa kilimo hapa Nchini wanazitumia vizuri takwimu kutoka NBS kwa minajili ya kuwatambua na kuwahudumia wakulima wote kwa ufanisi”, Amesema Mavunde.

Mavunde amesema ipo haja kwa serikali za Afrika kuzitumia miundombinu ya kisasa ili kupata Takwimu stahiki kwa lengo la kuboresha na kuhuisha sekta ya Kilimo ambayo ni sekta mama ya uzalishaji Barani Afrika.

“Nazikumbusha serikali za Afrika kuhakikisha wanawajengea uwezo taasisi za kukusanya takwimu kuwa za kisasa ili kufikia lengo la kuzalisha Takwimu za Kilimo zilizo bora na kupatikana kwa wakati na kukidhi mahitaji yatakayosaidia kukuza kilimo Afrika”, Mavunde

Aidha ametoa wito kwa shirika la Takwimu nchini (NBS) kijikita zaidi kwenye utafiti na uvumbuzi wa teknolojia za Kilimo ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo kwa kiasi kikubwa yanaathiri wakulima wengi hali itakayopelekea kutatiza mpango wa Kilimo kukua kwa asilimia 10 ifikapo 2030.

Kwa upande wake Afisa wa Sensa kwa mwaka 2022 Anna Makinda ameziasa taasisi na wadau wa maendeleo kuzitumia takwimu za sensa kuwafikia Wananchi kwa kuwatimizia mahitaji mbalimbali ya kijamii na kiuchumi kwani taarifa zao zimeanisha maeneo yote muhimu kwa kuzingatia idadi ya watu katika mikoa yote hapa Nchini.

Siku ya Takwimu Afrika huadhimishwa kila tarehe 18 Novemba ya kila mwaka lakini kila nchi inaweza kusherehekea kulingana na ratiba yake na kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka husika.

Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde akizindua mfumo wa Takwimu kiganjani ambao utawawezesha wananchi kupakua na kujionea takwimu za sensa popote alipo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!