Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akizungumza wakati akizindua Bodi ya Kituo Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC), Machi 6, 2026 jijini Dar es Salaam.
Na; Mwandishi Wetu,Dar es Salaam.
Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni ametoa maagizo matano kwa Bodi ya Kituo Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) kilichopo Morogoro mara baada ya kuizindua bodi hiyo.
Waziri Masauni ametoa maagizo hayo Machi 6, 2026 wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo jijini Dar es Salaam akieleza imepaswa kuimarisha mifumo ya kitaifa ya Upimaji, Utoaji Taarifa na Uhakiki wa gesijoto (MRV) ili kuhakikisha kuwa taarifa za kaboni nchini zinakuwa sahihi, za kuaminika na zinazokubalika kimataifa.
Pia ameielekeza Bodi hiyo kuhakikisha Miradi yote ya kaboni inayotekelezwa nchini inasimamiwa kwa ufanisi, uwazi na kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa pamoja na maslahi mapana ya Taifa.
Mhe. Masauni ameongeza kuwa bodi inapaswa kuweka Mazingira wezeshi yatakayovutia uwekezaji wa ndani wa kimataifa katika Sekta ya Kaboni huku ikihakikisha kuwa uwekezaji huo unalinda rasilimali za Taifa na kuleta manufaa ya kweli kwa wananchi, kuhakikisha kunakuwepo mfumo wa haki na uwazi wa mgawanyiko wa manufaa ili jamii zinazohifadhi rasilimali za asili zinufaike moja kwa moja na Miradi ya Kaboni inayotekelezwa katika maeneo yao.
“Kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika mifumo ya kimataifa ya biashara ya Kaboni hususan chini ya Ibara ya 6 ya Mkataba wa Paris, ikiwemo mifumo ya soko la Kaboni ili kuongeza fursa za kiuchumi kwa Taifa letu.
Aidha, ameisisitiza Bodi hiyo kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha Kituo hicho kinaendeshwa kwa uwajibikaji, uadilifu na weledi wa hali ya juu ili kuhakikisha mifumo ya Usimamizi wa Sekta ya Kaboni inalinda kikamilifu maslahi ya Taifa.
“Ni matarajio ya Serikali kuona kituo hiki kinakuwa kitovu cha ubora katika maswala ya ufuatiliaji wa Kaboni, biadhara ya Kaboni na Tafiti za mabadiliko ya tabianchi katika ukanda wa Afrika. Haya ni matarajio makubwa kwa taifa letu na yanahitaji Usimamizi madhubuti wa taasisi, mifumo imara ya ufuatiliaji pamoja na ushirikiano wa wadau wote.” Amesema Mhe. Masauni.
Ameongeza kuwa matarajio ya Serikali yaliyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, na Mpango wa muda mrefu wa Utekelezaji wake, sekta ya Kaboni inauwezo wa kuchangia takribani Dola za kimarekani bilioni mbili kwa Mwaka katika uchumi wa Taifa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi, Dkt. Albina Chuwa amesema ushirikiano ndio jambo la msingi katika kufikisha lengo na ndoto za watanzania, hivyo watajitahidi kutafuta fursa ili kupata matokeo mazuri.
“Ushirikiano wa kutosha ndio naomba kutoka kwa kila mmoja wetu kwani haya yote tunayoyazungumza tutakuwa tunafanya kazi nyepesi katika kuhakikisha kituo chetu cha Kaboni kinafanya vizuri,” amesema Dkt. Albina.
Amesema Uzinduzi wa Bodi unakuja katika kipindi muhimu ambacho sekta ya biashara ya kaboni inaendelea kukua kwa kasi duniani na hapa nchini, NCMC ina jukumu muhimu la kuhakikisha kuwa rasilimali za kaboni za nchi yetu zinasimamiwa kwa uwazi, weledi na kwa kuzingatia mifumo na viwango vinavyokubalika kimataifa.
Wajumbe wanaounda Bodi hiyo ni Bw. Khamis Hamza Khamis, Bi. Amne Sued Kagasheki, Bi. Farhat Mabrouk, Dkt. Ladislaus Kyaruzi, Bw. Rishad Bade pamoja na Dkt.Philipina Fenest Shayo.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akizungumza wakati akizindua Bodi ya Kituo Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC), Machi 6, 2026 jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya NCMC, Dkt. Albina Chuwa (kushoto kwake), Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt, Festo Dugange, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi (kulia kwake) na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais, Balozi Baraka Luvanda, mara baada ya uzinduzi wa Bodi ya Kituo Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC), Machi 6, 2026 jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akimpongeza Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC, Dkt. Albina Chuwa mara baada ya uzinduzi wa Bodi hiyo, Machi 6, 2026 jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Festo Dugange akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Kituo Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC), Machi 6, 2026 jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Kituo Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC), mara baada ya uzinduzi wa Bodi hiyo, Machi 6, 2026 jijini Dar es Salaam.
PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS








