
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), amesema jitihada za Serikali katika kufufua viwanda Mkoani Tanga zimeanza kuzaa matunda, akitolea mfano Kiwanda cha African Hamon ambacho kilikuwa hakifanyi kazi kabisa, lakini sasa kimeanza kufanya kazi na tayari kimeajiri zaidi ya vijana 200 kwa ajira za kudumu, jambo linalosaidia kuongeza ajira.
Waziri Kapinga amebainisha hayo Januari 6, 2026, wakati wa ziara yake ya kuona maendeleo na utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyoyatoa wakati wa ziara yake mkoani humo, likiwa na lengo la kurejesha hadhi ya Mkoa wa Tanga kuwa mkoa wa viwanda kama awali.

Amesisitiza kuwa lengo la wizara ni kuhakikisha viwanda vyote vilivyolengwa vinaanza kufanya kazi kikamilifu, ili kuimarisha soko la ndani na nje ya nchi kupitia bidhaa zinazozalishwa hapa Tanzania, ambapo baadhi ya viwanda, ikiwemo kiwanda cha Nondo cha Steel Rolling, kimeanza majaribio, na Kiwanda cha kutengeneza bidhaa za mbao cha Ply and Panel ambacho kimeanza ukarabati.
Waziri Kapinga pia amesema Serikali itaweka mwakilishi katika kila kiwanda ili kusaidia kurahisisha utatuzi wa changamoto za wawekezaji na kuhakikisha kipaumbele kinatolewa kwa haraka.
Aidha, Waziri Kapinga amesema juhudi hizi zinaendana na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, huku viwanda hivyo vikichangia moja kwa moja kuboresha maisha ya wananchi kupitia ajira za uhakika. Mpango huo umeelezwa wazi katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025–2030 na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, inayolenga kukuza uchumi wa viwanda na maendeleo endelevu.

Akizungumza, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Dkt. Batilda Burian, amesema kuwa kilio cha muda mrefu cha mkoa huo kilikuwa ni viwanda, kwani awali vilibaki kama magofu. Sasa wanafurahi kuona viwanda vikifufuliwa na ameahidi kuendelea kufuatilia ili kufungua viwanda vipya kila wilaya.
Aidha, amesema Serikali itasisitiza kuhakikisha Tanga inakuwa mkoa wa viwanda. Pia ameitaka Serikali kuongeza gati ya pili bandarini ili kurahisisha huduma za meli nyingi kutua bandarini, huku wakitarajia kufanya mkutano mkubwa wa kunadi fursa zilizopo mkoani humo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini, Mhe. Kassim Makuberi, amesema sasa wananchi wa Tanga wanakwenda kunufaika na uwepo wa fursa kutokana na uwepo wa viwanda hivyo. Amewahimiza wananchi kuchangamkia fursa hizo na wamiliki wa viwanda ambavyo havijafufuliwa kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha viwanda vyote vinaweza kufanya kazi.








