Na Chedaiwe Msuya, Dodoma
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), amesema katika jitihada za kudhibiti utoroshwaji wa mazao na bidhaa nchini, Serikali imeboresha mpaka kati ya Tanzania na Zambia. Amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Mapato Zambia (ZRA) ziliingia makubaliano (MoU) yenye lengo la kuchukua hatua mbalimbali za kulinda utoroshwaji huo.
Haya yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge Mhe. Condester Sichalwe (MOMBA) ambaye alitaka kujua ni lini Serikali itaboresha mpaka kati ya Zambia na Tanzania ili kudhibiti njia za panya ambazo mazao na bidhaa hutoroshwa bila kulipiwa kodi.
Mhe. Chande alisema kwamba ZRA na TRA zimeingia makubaliano ya kuboresha mfumo wa uondoshaji mizigo TANCIS, ambao sasa umeshikamana na mfumo wa ASYCUDA World wa Zambia ili kurahisisha taratibu za uondoshaji mizigo na kubadilishana taarifa.
“Serikali pia imesimika midaki (baggage and cargo scanners) za kukagua mizigo inayobebwa na abiria pamoja na magari,” aliongeza Mhe. Chande.
Aidha, aliongeza kuwa Serikali ya Zambia inapanua barabara na eneo la maegesho upande wa Nakonde ili kupunguza msongamano katika mpaka wa Tunduma.
Pia, alisema Serikali inaendelea kubainisha vihatarishi katika magari ya mizigo yanayovuka mpaka kati ya Tanzania na Zambia.
Sambamba na hayo, Mhe. Chande alisema kwamba Serikali kupitia TRA inaendelea kuimarisha doria ili kudhibiti maeneo yote ya mpaka wa Tanzania na Zambia kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ili kulinda mapato ya serikali.