Home Kitaifa KAMISHNA WA MADINI APONGEZA TAWOMA KUREKEBISHA KATIBA

KAMISHNA WA MADINI APONGEZA TAWOMA KUREKEBISHA KATIBA

Kamishna wa Madini Dkt. Abdalrahaman Mwanga amekipongeza Chama cha Wanawake Wachimbaji Madini Tanzaniza (TAWOMA) baada ya kufanya marekebisho ya Katiba na Kanuni zinazo kiongoza chama hicho baada ya kuonekana Katiba ya awali ina mapungufu.

Dkt. Mwanga ametoa pongezi hizo wakati akizindua Marekebisho ya Katiba na Kanuni za TAWOMA uliofanyika katika ukumbi wa African Dream jijini Dodoma.

“Naomba nichukue fursa hii kuwapongeza sana, hatua hii inaonesha ni namna gani TAWOMA ipo tayari kwa mabadiliko ili kujiimarisha zaidi,” amesema Dkt. Mwanga.

Aidha, Dkt. Mwanga ametumia fursa hiyo kukitaka chama hicho kuchangamkia fursa zilizopo kwenye Sekta ya Madini ambapo amesema sekta hiyo inatoa fursa nyingi za ajira kupitia kazi mbalimbali za utafutaji wa madini, uchimbaji, uchenjuaji usafishaji wa madini pamoja na biashara ya madini.

Sambamba na uzinduzi huo, Dkt. Mwanga pia amezindua Bodi ya TAWOMA yenye wajumbe saba ambapo amewataka kusimamia shughuli zote za chama hicho kwa umakini ili kukiwezesha kudhibiti na kusimamia rasilimali za chama hicho.

Dkt. Mwanga amesema Wizara ya Madini inaendelea kusimamia Sheria na Kanuni za madini ili kuhakikisha inawezesha na kuongeza ushiriki wa nchi na wananchi ikiwemo TAWOMA katika shughuli za sekta ili kukuza uchumi wa nchi.

Pia, Dkt. Mwanga amewataka wanachama wa TAWOMA kuhakikisha wanashirikiana na watanzania wengine kuchangamikia fursa na kushiriki ipasavyo katika shughuli za madini ili waweze kukuza uchumi wao na kunufaika na rasilimali madini.

Naye, Mwenyekiti wa TAWOMA Semen Malale amesema maamuzi ya kufanya mabadiliko ya Katiba na kuanzisha Bodi ya TAWOMA yamefanyika ili kuimarisha chama hicho na kuhakikisha wanawake wanakuwa mstari wa mbele katika kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kujenga taifa.

Vile vile, Malale amesema TAWOMA inampango wa kuungana na wanawake wote waliopo kwenye mnyororo mzima wa thamani wa madini ili kuwa na sauti moja katika kujiletea maendeleo.

Pia, Malale amesema chama kina dhamira ya kuanzisha Saccos Maalumu itakayowezesha Wanawake waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa madini waweze kupata mitaji ili kuendesha shughuli zao kwa uhakika zaidi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!