Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linaendelea kuwahakikishia hali ya usalama wafanyabiashara waliofungua maduka yao na kuendelea na kazi kwa kuongeza doria mtaani.
Mapema hii leo, Juni 26, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishina wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa, akiwa kwenye doria, amefika mtaa wa Lumumba na kuzungumza na baadhi ya wananchi na wafanyabiashara wa eneo hilo na kuwaondolea hofu ya kiusalama wale wote waliofungua maduka yao.
“Mtu anafunga duka lake eti anaogopa mtu mwingine kumfanyia fujo asifanye biashara yake vizuri, doria yetu imelenga kuwaondolea hofu ya aina yoyote. Kama mkoa ulivyokuwa salama, sisi Jeshi la Polisi tunaendelea kujipanga kwa kuongeza askari watakaokuwa kwenye doria za magari, za miguu na pikipiki,” amesema Kamanda Mutafungwa.
“Wafanyabiashara ambao wameanza kufungua maduka, sisi tunahimiza wafungue kwa sababu hawatafanyiwa kitu chochote kibaya na mtu yeyote. Sisi ndivyo tulivyojipanga hivyo kusiwe na visingizio vyovyote vya kukosa usalama katika mkoa wetu,” amesisitiza Kamanda Mutafungwa.
Aidha, Kamanda Mutafungwa amewataka wafanyabiashara wanaotishiwa wasifungue maduka yao watoe taarifa Polisi ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa haraka.