
JUBILEE Group Tanzania imezindua rasmi ukuta uliojengwa kuzunguka Shule ya Msingi Madenge iliyopo Temeke, Dar es Salaam, kwa lengo la kuimarisha usalama na kuondoa changamoto ya usumbufu uliokuwa ukisababishwa na wapita njia, hali iliyokuwa ikiathiri mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia.
Kupitia ujenzi wa ukuta huo, taasisi hiyo inaamini kuwa shule itanufaika na mazingira salama na tulivu yatakayowawezesha walimu kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi, huku wanafunzi wakipata mazingira bora ya kujifunza na kufanya vizuri kitaaluma.
Uzinduzi huo umefanyika leo, Agosti 7, 2026, katika Shule ya Msingi Madenge na kuhudhuriwa na Maofisa Watendaji Wakuu wa Jubilee Life Insurance na Jubilee Health Insurance, Bi. Helena Mzena na Dkt. Harold Adamson, pamoja na viongozi wa serikali za mitaa, uongozi wa shule na wafanyakazi wa Jubilee Group Tanzania.
Jubilee Group Tanzania imesisitiza kuwa itaendelea kutekeleza shughuli za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kwa lengo la kuchangia maendeleo katika sekta za elimu, afya na ustawi wa jamii, kwa kuamini kuwa jamii yenye maendeleo ndiyo msingi wa maendeleo endelevu ya taifa.
Akisoma risala ya Shule ya Msingi Madenge, Mwalimu Edith Mchome amesema shule hiyo inatoa shukrani za dhati kwa Jubilee Life Insurance kwa kujenga ukuta huo, ambao umeondoa changamoto nyingi zilizokuwa zikiwakabili walimu na wanafunzi kutokana na kukosekana kwa uzio.
“Kwa niaba ya wanafunzi wote wa Shule ya Msingi Madenge, tunatoa shukrani zetu za dhati kwa Jubilee Life Insurance kwa kuiwezesha shule yetu kujengewa uzio katika upande uliokuwa na changamoto kubwa. Hapo awali hatukuweza kusoma kwa utulivu kutokana na usumbufu uliokuwa ukitokea mara kwa mara,” amesema Mchome.
Ameongeza kuwa ujenzi wa uzio huo umerejesha utulivu na usalama shuleni, huku ukiondoa kabisa vitendo vya usumbufu kutoka kwa wapita njia na watu waliokuwa wakivamia eneo la shule.
“Kabla ya kujengwa kwa ukuta huu kulikuwa na vurugu za wapita njia na hata watu waliokuwa wakivamia mazingira ya shule. Sasa tuko salama na wanafunzi wanaweza kujifunza katika mazingira yenye utulivu,” amesema.
Aidha, Mchome amesema Jubilee Life Insurance imechangia pia kuboresha mazingira ya shule kwa kupanda miti iliyosaidia kuhifadhi mazingira, kutoa kivuli, kupunguza athari za upepo mkali na kuboresha upatikanaji wa hewa safi kwa walimu na wanafunzi.
Mbali na hilo, amesema taasisi hiyo imeipatia shule vifaa vya usafi, ikiwemo reki, majembe na fyekeo, ambavyo vinaendelea kusaidia kutunza usafi wa mazingira ya shule kila siku.









