

Mgombea ubunge wa Jimbo la Kisarawe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Selemani Saidi Jafo, ameahidi kuendeleza miradi ya maendeleo kwa kasi zaidi katika kipindi cha miaka mitano ijayo, akitaja kipaumbele chake kuwa barabara, shule, maji, umeme, afya, mawasiliano na usalama wa wananchi.
Akizungumza na wakazi wa Mafizi, Dkt. Jafo alisema serikali imeanza kutatua changamoto nyingi za miundombinu na sasa wananchi wanaona matunda ya jitihada hizo.

Dkt. Jafo alisema tayari madaraja 23 yamejengwa katika sekta ya barabara, na dhamira yake ni kuhakikisha barabara zinapitika mwaka mzima bila kikwazo hata mvua zinaponyesha.
“Miaka mitano ijayo nitahakikisha tunapata majibu ya kudumu ili mvua ikinyesha magari yaendelee kupita. Barabara zitabaki kuwa kipaumbele changu kikubwa,” alisema.
Alibainisha kuwa changamoto ya umeme imeanza kufanyiwa kazi, na tayari umeme umefika kutoka Mzenga hadi Dororo. Dhamira yake ni kuhakikisha vitongoji vya Mkundi na Tazara vinapata umeme pamoja na maji ya uhakika.
Dkt. Jafo alisema miradi ya elimu imepewa msukumo, ambapo madarasa mapya manane yamejengwa Kisarawe kwa msaada wa Rais Samia Suluhu Hassan. Pia shule mpya ya msingi Vizenbe na Masimba zitajengwa ili kupunguza changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu.
Katika afya, alisema wodi ya kinamama itajengwa na wataalamu wa afya kuongezwa ili kuongeza ufanisi wa huduma.
Akizungumzia sekta ya mawasiliano, Dkt. Jafo alisema, “Zamani hatukuwa na mawasiliano, sasa yapo na yataendelea kuimarishwa.” Aidha, aliwahimiza wananchi kuimarisha michezo katika vitongoji husika ili kukuza vipaji na mshikamano wa jamii.
Kuhusu kilimo, Dkt. Jafo alisema juhudi zinaendelea kudhibiti wanyama waharibifu wa mazao. Kwa upande wa ufugaji, aliahidi kuanzisha majosho ya mifugo ili wafugaji wafuge kwa ufanisi.
Vilevile, alisema kituo kidogo cha polisi kitajengwa katika eneo la Gwata ili kuimarisha ulinzi na usalama wa wananchi.

Naye mgombea udiwani wa kata hiyo, Bora Mohamed Mmayage, aliahidi kushirikiana na Dkt. Jafo kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa vitendo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kisarawe, Shabani Sika, aliwataka wananchi kuendelea kuamini chama hicho na kutojiingiza katika propaganda za wanaodai hakuna maendeleo.
“Yeyote anayedai hakuna kilichofanyika ni adui wa maendeleo,” alisema.
Aliwaomba wananchi kumpigia kura za ndiyo mgombea Urais, Ubunge na Udiwani ili kuendeleza kasi ya miradi.
