Na Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza kufuta leseni ya rejareja ya bidhaa za mafuta ya petroli ya kampuni ya Iyan Energy Limited na kusitisha kwa muda wa miezi sita leseni ya kampuni ya Crescent Energy Tanzania Limited, baada ya kubaini ukiukwaji wa sheria na masharti ya leseni.
Kwa mujibu wa taarifa ya EWURA, uamuzi huo umefanyika kufuatia maamuzi yaliyotolewa na Bodi ya Wakurugenzi wakati wa vikao vyake vya hivi karibuni.
EWURA imesema leseni iliyofutwa ni Petroleum Retail Licence Na. PRL-2018-269, iliyokuwa ikimilikiwa na Iyan Energy Limited kwa ajili ya kuendesha biashara ya rejareja ya mafuta katika Kiwanja Na. 26 na 27, Barabara ya Pangani, Jiji la Tanga.
Wakati huohuo, Bodi imesitisha kwa muda wa miezi sita leseni ya rejareja ya bidhaa za mafuta ya petroli Namba PRL-2022-296 ya Crescent Energy Tanzania Limited, iliyotolewa kwa ajili ya kuendesha biashara ya rejareja katika Kiwanja Na. 5, Kitalu “N”, Eneo la Chamakweza, Wilaya ya Chalinze, Mkoa wa Pwani.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa maamuzi hayo yamefanyika baada ya EWURA kujiridhisha kuwa kampuni hizo zilikuwa zikijihusisha na shughuli zinazofanana na biashara ya uuzaji wa bidhaa za mafuta kwa jumla, hali ambayo haikuruhusiwa chini ya leseni za rejareja walizokuwa nazo.
EWURA imeeleza kuwa hatua hizo zinakiuka Kifungu Na. 131 cha Sheria ya Petroli, Sura ya 392, pamoja na Kanuni ya 9 na 11 za Kanuni za Mafuta (Biashara ya Jumla, Uhifadhi, Rejareja na Matumizi Binafsi), Tangazo la Serikali Na. 150/2022.
Onyo kwa umma
Katika taarifa yake, EWURA imeutaarifu umma kuwa kujihusisha kwa namna yoyote na kampuni hizo katika biashara ya usambazaji wa bidhaa za mafuta ya petroli kutakuwa kinyume cha sheria, na kwamba hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka.
Mamlaka hiyo imeongeza kuwa itaendelea kusimamia sekta ya mafuta kwa kuhakikisha kunakuwa na mazingira ya ushindani wa haki na upatikanaji wa uhakika wa bidhaa za mafuta nchini, kwa kudumisha “uwanja ulio sawa” kwa wadau wote.








