Home Kitaifa DKT. SEIF AAGIZA KUKAMATWA MKANDARASI NJOMBE AKISHINDWA KUKAMILISHA KAZI KWA WAKATI

DKT. SEIF AAGIZA KUKAMATWA MKANDARASI NJOMBE AKISHINDWA KUKAMILISHA KAZI KWA WAKATI

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Jafar Seif, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Juma Sweda, kuwa endapo mkandarasi Hamerkop International Limited anayejenga jengo la wagonjwa wa nje (OPD) katika Hospitali ya Mji Njombe (Kibena) atashindwa kukamilisha ujenzi wa jengo hilo kabla ya Februari 8, 2026, akamatwe na kuhojiwa kwa hatua zaidi za kisheria.

Naibu Waziri Dkt. Seif ametoa agizo hilo leo Januari 7, 2026, alipofanya ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa jengo hilo lenye ghorofa moja, linalotarajiwa kutumika kutolea huduma kwa wagonjwa wa nje, wagonjwa wanaohitaji mionzi, wagonjwa mahututi, huduma za meno na ofisi za idara nyingine ndogondogo, ikiwa ni uboreshaji wa mazingira ya utoaji wa huduma na bima.

Dkt. Seif amesema msingi wa maelekezo yake ya kukamatwa kwa mkandarasi huyo ni kutokana na kuongezewa muda mara mbili nje ya muda wa mkataba halisi kati yake na Serikali, lakini bado mwenendo wa ujenzi wa jengo hilo unaonekana kuzorota, hatua inayochelewesha utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi, licha ya Serikali kumlipa mkandarasi kiasi cha shilingi milioni 784.2 kati ya shilingi milioni 863.3 ambazo ni thamani ya mradi mzima hadi kukamilika.

Licha ya ripoti ya mshauri wa mradi kutoka Ofisi ya Wakala wa Majengo (TBA), Bw. Kenan Lyimo, kuonesha kuwa ujenzi wa jengo hilo uko asilimia 70, mkandarasi Hamerkop International Limited amedai kuwa muda uliosalia unatosha kutekeleza hatua zote za ujenzi na kukabidhi mradi huo kwa Serikali ndani ya kipindi cha muda wa pili wa nyongeza aliopewa, ambao ni Februari 8, 2025.

Hospitali ya Mji Njombe Kibena inahudumia jumla ya watu 204,247 kwa mwaka, miongoni mwa wagonjwa hao wanatoka halmashauri zote za Mkoa wa Njombe, ikiwemo Mji Njombe, Wilaya ya Njombe, Wanging’ombe, Mji Makambako, Makete na Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa.

Naibu Waziri Dkt. Seif yuko mkoani Njombe kwa ziara maalum ya kikazi ya siku tatu kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali inayolenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, hususan kada ya afya ngazi ya msingi, ikiwa ni kuelekea utekelezaji wa mpango wa huduma ya Bima ya Afya kwa Wote.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!