
Mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita, wamefanikiwa kujenga vituo vinne vya kukusanya na kuchakata mazao ya nyuki mkoani Katavi ili kuimarisha ufugaji wa nyuki na kuongeza uzalishaji wa asali katika mkoa huo.
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Oktoba 18, 2025, katika viwanja vya Azimio mjini Mpanda, Dkt. Samia aliahidi kuendeleza uwekezaji katika sekta ya ufugaji nyuki na kuijumuisha katika Mpango wa “Jenga Kesho Iliyobora” ili kuwahamasisha vijana kushiriki zaidi katika sekta hiyo.

Amesema pia kuwa serikali yake itaendelea kutoa ruzuku za mbolea na pembejeo za kilimo, kujenga skimu za umwagiliaji na maghala ya kuhifadhia chakula kwa ajili ya kuongeza uzalishaji, hasa katika mikoa ya Katavi na Rukwa ambayo ni wazalishaji wakubwa wa mazao ya chakula.
Dkt. Samia ameongeza kuwa serikali itaendelea na ujenzi wa mabwawa, vizimba na vituo vipya vya ukuzaji wa viumbe maji na samaki katika Ziwa Tanganyika, huku akiwataka vijana kujipanga vizuri kutumia fursa zitakazotokana na miradi hiyo endapo ataendelea kuiongoza serikali baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.