
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Alhamisi Oktoba 16, 2025, anaendelea na kampeni zake za Uchaguzi Mkuu katika Viwanja vya Kaitaba, Bukoba Mjini, Mkoa wa Kagera. Katika mkutano huo, anatarajiwa kunadi Ilani ya CCM, kueleza mafanikio ya serikali ya awamu ya sita, na kuomba ridhaa ya kuongoza kwa muhula mwingine.

Jana Jumatano, Dkt. Samia alianza kampeni zake mkoani humo kwa kufanya mikutano katika maeneo ya Muleba, Kyaka na Kayanga. Miongoni mwa ahadi alizotoa ni pamoja na ujenzi wa uwanja wa ndege Missenyi, ugawaji wa mbegu za parachichi na kahawa, utoaji wa ruzuku ya mbolea na pembejeo za kilimo, uwezeshaji wa sekta ya uvuvi, usimamizi wa kilimo cha vanila, pamoja na kuendeleza utoaji wa huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya na usambazaji wa umeme vijijini.
Kwa mujibu wa Ilani ya CCM anayoinadi kwa Bukoba Mjini, ndani ya miaka mitano ijayo, chama hicho kimeahidi kujenga Hospitali ya Wilaya, vituo vya afya na zahanati katika kila kata na kijiji, kukamilisha ujenzi wa kituo cha afya Kagondo, kujenga shule ya kata, madarasa 131, kukarabati shule kongwe nne, kujenga nyumba za walimu na mabweni mawili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule za msingi za Manispaa ya Bukoba.

Pia, Ilani hiyo imeainisha mpango wa kujenga madarasa 28, maabara 11, maktaba na nyumba nne za walimu kwa shule za sekondari. Aidha, CCM imepanga kujenga masoko matano katika maeneo ya Machinjioni, Kagondo, Rwamishenye, Kashai na Kyabitembe, pamoja na kitega uchumi katika eneo la Mayunga.
Katika sekta ya miundombinu, ndani ya kipindi hicho, CCM imepanga kuimarisha bandari ya Kemondo na kuboresha barabara za ndani ya Manispaa ya Bukoba.
Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa serikali ya awamu ya sita, Wilaya ya Bukoba imenufaika kwa kujengewa hospitali mbili (Bukoba DC na Manispaa), shule za msingi na sekondari kujengwa na kukarabatiwa, upatikanaji wa maji safi na salama vijijini kuongezeka kutoka asilimia 76 hadi 83, ujenzi wa bandari ya Bukoba, uendelezaji wa kituo kikuu cha mabasi, ujenzi wa barabara ya njia nne mjini Bukoba na kuendeleza soko kuu la Manispaa.