
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kuwa ikiwa atachaguliwa kuongoza Tanzania katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, pamoja na mambo mengine atatia mkazo zaidi katika utoaji wa ruzuku za mbolea, pembejeo na chanjo kwa wakulima na wafugaji wa Tanzania.
Dkt. Samia amebainisha hayo leo Ijumaa Septemba 12, 2025 mbele ya wananchi wa Ipuli Mkoani Tabora wakati akihitimisha mikutano yake ya kampeni Mkoani humo akisisitiza pia kuendelea kuboresha minada, kujenga minada mipya pamoja na ujenzi wa majosho kwaajili ya wafugaji wa Mkoa wa Tabora.

Dkt. Samia pia ameahidi ikiwa atachaguliwa atamaliza changamoto na kero za Maji zilizopo Mkoani humo, akisema dhamira yake ni kuhakikisha Mkoa huo na Tanzania kwa ujumla inakuwa na maji ya uhakika kwa kila Mtanzania popote kule alipo.
“Najua ndani ya Wilaya ya Sikonge tumefikia asilimia 67 lakini bado zipo changamoto ila kuna miradi mingi inaendelea kutekelezwa na itakapokamilika tunatarajia Mkoa wa Tabora uwe una maji ya kutosha na kwamba kila mwana Tabora ana maji ya kutosha na mradi wa Maji wa Ziwa Viktoria na wa Miji 28 utamaliza dhiki ya Maji ndani ya Mkoa wa Tabora.” Amesema Dkt. Samia.

Kadhalika Dkt. Samia ametoa wito kwa Vijana wa Mkoa huo kujiandaa kutumia vyema fursa za ajira zinazotokana na ujenzi wa miradi mikubwa ya Kitaifa iliyopita Mkoani Tabora ikiwemo ujenzi wa Bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima Nchini Uganda kwenda Chongoleani Mkoani Tanga, akisema miradi hiyo imekuwa ikizalisha ajira nyingi wakati wa ujenzi wake.








