
Rais wa Awamu ya Sita na Mgombea wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka msisitizo katika kampeni zake kuwa njia kuu ya kuwawezesha wananchi kuongeza kipato na kupunguza umaskini ni kupitia uongezaji wa fursa za ajira na shughuli za kiuchumi.
Ameahidi kuweka mazingira bora ya kuzalisha ajira kwa vijana, wanawake, watu wenye ulemavu na wazee, akilenga kuzalisha ajira zenye tija zisizopungua milioni nane katika sekta rasmi na isiyo rasmi, nusu yake ikiwa katika sekta rasmi.

Ili kufanikisha hilo, Serikali yake itaanzisha programu za ujenzi wa miundombinu ya kongani za viwanda vidogo na vya kati katika kila mkoa na wilaya, kwa lengo la kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, uvuvi, ufugaji, misitu na madini, sambamba na kuweka mazingira rafiki ya kikodi kwa kongani hizo.
Ilani ya CCM 2025/2030 pia imepanga kuanzisha dirisha maalumu la mitaji kwa kampuni changa, maeneo ya kukuza bunifu na teknolojia, na vituo vya mafunzo stadi kwa vijana watakaoandaliwa kushindana kupata ajira nje ya nchi.

Aidha, mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi itapitiwa upya ili kuwa na mfumo mmoja imara wenye kuhudumia makundi yote, huku ikianzishwa programu za mafunzo na hamasa za kutumia fursa za ajira nje ya nchi.
Dkt. Samia ameongeza kuwa Serikali itahamasisha uanzishwaji wa makampuni ya vijana na vyama vya ushirika vya kibiashara katika halmashauri zote nchini, ili viweze kupata mikopo, mitaji na nyenzo za kujiajiri na kutoa ajira kwa wengine, hususan wahitimu wa elimu ya juu.