
Na Shomari Binda-Musoma
SHILINGI bilioni 30 zinazo tekeleza mradi wa maji taka manispaa ya Musoma zinatarajia kuuweka mji huo katika hali ya usafi.
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka alipotembelea eneo la mradi kukagua shughuli zinazo fanyika.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutawanya wananchi wa manispaa ya Musoma kuunganishwa na mradi huo kuelekeza maji taka wanayo zalisha.
Chikoka amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na shirika la maendeleo la Ufaransa kwa mradi huo kwaajili ya kuweka mji wa Musoma kwenye hali ya usafi.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema kupitia mradi huo vyoo zaidi ya 370 vimejengwa kwenye shule na maeneo ya mikusanyiko ya watu kwaajili ya kutoa huduma.
” Tunamshukuru sana Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwaajili ya mradi huu ambao sasa unakwenda kuweka mji wetu safi kutokana na maji taka yanayozalishwa.
” Kupitia mradi huu wananchi wataunganishwa kwenye mfumo na kuhakikisha maji taka yote yanayo zalishwa yanaelekezwa eneo la mradi”,amesema.
Kwa upande wake mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) mhandisi Nicas Mugisha amesema matokeo ya mradi huo ni kukamilika kwa mradi wa awali wa maji safi.
Amesema hatua ya awali mradi huo utahudumia maeneo ya katikati ya manispaa ya Musoma na baadae utatanuka pembezoni mwa mji.
Nicas amesema majaribio ya mradi huo yanatarajiwa kufanyika mwezi wa 4 na kudai shughuli za utekelezaji wa mradi zinakwenda vizuri.
