Home Kitaifa BALOZI KINGU ASISITIZA UBORA WA VIFAA NA KUONGEZA NGUVU KAZI KATIKA MIRADI...

BALOZI KINGU ASISITIZA UBORA WA VIFAA NA KUONGEZA NGUVU KAZI KATIKA MIRADI YA REA

🔹 Lengo ni kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati

Na Veronica Simba, SONGEA

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu amewaagiza Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini wilayani Songea, kuzingatia matumizi ya vifaa vyenye ubora na kuongeza nguvu kazi ili miradi hiyo ikamilike kwa muda uliopangwa.

Balozi Kingu pia amewataka Wakandarasi kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia usalama wa miradi wanayoitekeleza ili azma ya Serikali kuhakikisha inawanufaisha wananchi iweze kutimizwa.

Amesema hayo leo Novemba 19, 2023 alipokuwa akizungumza na Wakandarasi kutoka kampuni ya White City na Namis Corporate Ltd ambao wanatekeleza miradi ya umeme vijijini wilayani Songea.

“Nawasisitiza mtembee katika ratiba tuliyokubaliana kwani mkikamilisha miradi kwa wakati na ubora ni sifa kwenu pia na historia itaandikwa kuwa mlichangia katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia upatikanaji wa nishati adhimu ya umeme,” amesema.

Akizungumzia takwimu za umeme vijijini kwa Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla, Balozi Kingu amesema jumla ya vijiji 442 kati ya 554 vimekwishafikishiwa umeme sawa na asilimia 79.8 na kwamba hadi kufikia mwishoni mwa Desemba mwaka huu, vijiji vyote vitakuwa vimefikishiwa nishati hiyo.

Akidadavua zaidi, amesema kuwa kwa Wilaya ya Songea, Mkandarasi Namis Corporate Ltd alipewa vijiji 165 ambapo hadi sasa amekwishawasha vijiji 82 na ifikapo Novemba 22 atakuwa amewasha vingine 25 hivyo kufikisha vijiji 107.

“Kati ya vijiji 58 ambavyo Namis atakuwa kabakiza tumekubaliana kuwa kufikia mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka huu atakuwa amewasha 44 na kufikia Desemba 30 atakuwa amewasha 18 vilivyobaki hivyo kukamilisha vijiji vyote.”

Kwa upande wa Mkandarasi White City, Mwenyekiti wa Bodi ameeleza kuwa alipewa vijiji 99 na mpaka sasa amewasha vijiji 77 na kubakiwa na 22. Hata hivyo, kati ya hivyo 22 vilivyobakia, 15 vitakuwa vimewashwa ifikapo Novemba 27 na 7 ifikapo Desemba 5 mwaka huu.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu ameeleza kuwa jumla ya miradi minne inatekelezwa mkoani Ruvuma ambapo serikali imetoa billioni 124 katika kutekeleza miradi hiyo.

Mhandisi Olotu alitaja miradi hiyo kuwa ni Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili unaogharimu shilingi bilioni 91.

Mingine ni Mradi wa Ujazilizi Fungu la Pili C unaogharimu shilingi bilioni 27, Mradi wa kupeka umeme katika migodi midogo ya madini (shilingi bilioni 5) pamoja na Mradi wa kupeleka umeme katika vituo vya afya na pampu za maji (shilingi bilioni moja.)

“Serikali imewekeza takribani shilingi bilioni 124 kwa ajili ya kupeleka umeme vijijini katika Mkoa wa Ruvuma kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi kupitia matumizi ya nishati hiyo katika shughuli mbalimbali za kiuchumi,” amefafanua Mhandisi Olotu.

Aidha, ameeleza kuwa kutokana na uwepo wa umeme vijijini, matokeo chanya yanaendelea kudhihirika ambapo takwimu zinaonesha kuwa idadi ya vijana waliokuwa wakikimbilia mjini imepungua kwa kiasi kikubwa na sasa wengi wao wanatoka mjini kurudi vijijini kwenda kujishughulisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo saluni za kunyoa, kazi za kuchomelea vyuma na nyinginezo.

Akizungumza kwa niaba ya Wakandarasi wenzake, Amran Othman kutoka kampuni ya Namis Corporate Ltd ameahidi kuwa watafanyia kazi maelekezo yote waliyopatiwa na watakamilisha miradi kwa wakati na ubora unaotakiwa.

Awali, Ujumbe huo ulikutana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Laban Thomas na kumweleza lengo la ziara hiyo kuwa ni kukutana na kujadiliana na Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini kuhusu namna ya kufanikisha kukamilisha miradi hiyo kwa wakati na ubora.

Mkuu wa Mkoa pamoja na kupongeza kazi nzuri inayofanywa na REA, alisisitiza Wakala kuwasimamia Wakandarasi ili wakamilishe kazi kwa wakati kwa kuzingatia kuwa msimu wa mvua umekwishaanza hivyo iwekwe mikakati itakayofanya mvua isiwe kikwazo.

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!