Home Biashara AFRIKA YAWEKA MIKAKATI YA KUHARAKISHA VIWANDA NA BIASHARA

AFRIKA YAWEKA MIKAKATI YA KUHARAKISHA VIWANDA NA BIASHARA

Na. Saidina Msangi, WF, Abidjan, Côte d’Ivoire.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mshamu Ali Munde (Mb), kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Pamoja wa 9 wa Kamati Maalum ya Mawaziri (STC) ya Umoja wa Afrika inayoshughulikia masuala ya Fedha, Uchumi, Mipango na Mtangamano, pamoja na Mkutano wa 5 wa Kamati ya Mawaziri wa Biashara, Utalii, Viwanda na Madini.

Mkutano huo wa kimkakati unalenga kuweka misingi imara ya ushirikiano wa kiuchumi barani Afrika.

Mkutano huo umejadili kwa kina umuhimu wa nchi za Afrika kuharakisha juhudi za kuendeleza sekta ya viwanda kwa kuongeza thamani ya malighafi za ndani badala ya kuzisafirisha zikiwa ghafi, kuimarisha minyororo ya thamani ya kikanda, pamoja na kuweka mazingira bora na wezeshi yatakayovutia uwekezaji wenye tija kiuchumi.

Wajumbe wa mkutano huo walibainisha kuwa, kutokana na Bara la Afrika kuwa na rasilimali nyingi za asili, ardhi kubwa yenye rutuba kwa ajili ya kilimo, madini ya kimkakati na idadi kubwa ya vijana ambao ndio nguvu kazi kuu katika uzalishaji, kuna umuhimu kwa Afrika kuwa kitovu cha uzalishaji na biashara duniani.

Aidha, mkutano huo umehimiza umuhimu wa kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuboresha usimamizi wa rasilimali za asili, na kupambana na ukwepaji wa kodi ili kukabiliana na pengo kubwa la ufadhili wa maendeleo ya miundombinu ya kisekta.

Mawaziri na wataalamu hao walikubaliana kuwa maendeleo ya viwanda hayawezi kufikiwa bila uwepo wa mfumo imara wa kifedha utakaowezesha upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu, kupunguza gharama za mikopo, na kuvutia sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika miradi ya maendeleo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!