
DAR ES SALAAM
KATIBU Mkuu wa Shirika la Wanawake la Kiafrika (PAWO), Dkt. Grace Kabayo, ameitaka jamii kuhakikisha wanawake wanashirikishwa kikamilifu katika maamuzi yanayohusu amani, usalama na maendeleo, akisisitiza kuwa wanawake si waathirika wa migogoro pekee bali ni viongozi na wajenzi muhimu wa amani.
Dkt. Kabayo ameyasema hayo jijini Dar es Salaam katika Jukwaa la Ushirikishwaji wa Asasi za Kiraia kuhusu Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama 2026, lililolenga kuimarisha ushiriki wa asasi za kiraia katika utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Wanawake, Amani na Usalama wa Tanzania wa mwaka 2025–2029.
Amesema mafanikio ya mpango huo hayatapimwa kwa kupitishwa kwake pekee, bali kwa utekelezaji wake na mabadiliko utakayoleta katika maisha ya wanawake na jamii.
“Kipimo halisi kitakuwa ni utekelezaji wake,” amesema.
Dkt. Kabayo amesema utekelezaji wa ajenda hiyo si jukumu la Serikali pekee, bali unahitaji ushirikiano wa asasi za kiraia, mashirika ya wanawake, vijana, taasisi za dini, wasomi, viongozi wa kimila na wadau wa maendeleo.
Amesema wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika kupatanisha migogoro, kuimarisha mshikamano wa jamii na kujenga amani, lakini bado wanakabiliwa na vikwazo vinavyowazuia kushiriki kikamilifu katika maamuzi rasmi ya amani na usalama.
Ametaka asasi za kiraia kuunganisha nguvu na kushirikiana katika utekelezaji wa ajenda hiyo, akipendekeza kuanzishwa kwa Mtandao wa Tanzania 1325 wa Asasi za Kiraia utakaosaidia uratibu, kubadilishana uzoefu, kufanya utetezi na kuimarisha uwajibikaji.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwapa nafasi wanawake vijana katika uongozi, ujenzi wa amani, ujasiriamali na matumizi ya teknolojia, akisema wao ni sehemu muhimu ya mustakabali wa amani na usalama nchini.
Kwa upande wake, Mshauri wa Sera wa Kikanda kuhusu Wanawake, Amani na Usalama wa UN Women, Bi. Idil Absiye, amesema utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa unapaswa kushushwa hadi ngazi za jamii ili Serikali za Mitaa, mashirika ya wanawake na viongozi wa jamii waweze kutambua changamoto za amani na usalama na kuzitafutia ufumbuzi.
Bi. Absiye amesema ushiriki wa asasi za kiraia ni muhimu katika kuzuia migogoro, kuimarisha mshikamano wa jamii na kukuza uongozi wa wanawake.
Amesema mafanikio ya Mpango Kazi huo yanapaswa kupimwa kwa mabadiliko halisi katika maisha ya wanawake na jamii, badala ya kuishia katika uwepo wa waraka pekee.









