



OFISI ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imezitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha zinabuni na kuandaa miradi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) katika bajeti ya mwaka wa fedha 2027/2028, ili kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika kuchangia na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI (Afya), Profesa Tumaini Nagu, wakati akifungua kikao cha maafisa bajeti wa mikoa na halmashauri kilicholenga kufanya tathmini ya uandaaji na utekelezaji wa mipango na bajeti katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Prof.Nagu amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayotegemea kwa kiasi kikubwa ushiriki wa sekta binafsi katika kuchochea uwekezaji na maendeleo ya kiuchumi nchini.
“Ni wajibu wa maafisa mipango na bajeti kuhakikisha wanabuni miradi inayoweza kutekelezwa kwa ubia na sekta binafsi pamoja na kuwashirikisha wadau wa maendeleo, badala ya kuendelea kutegemea fedha kutoka Serikali Kuu pekee.”amesema Prof.Nagu
Ameeleza kuwa matarajio ya Serikali ni kuona asilimia 80 ya maendeleo yanachochewa na sekta binafsi, hivyo ni muhimu mikakati hiyo kuanzia katika ngazi za halmashauri ili kufanikisha azma hiyo ya kitaifa.
Katika hatua nyingine, Prof. Nagu amewataka maafisa mipango na bajeti kuhakikisha maandalizi ya bajeti za halmashauri yanazingatia mwenendo wa mapato na matumizi ya miaka iliyopita, huku wakitathmini uendelevu wa vyanzo vya mapato kabla ya kutumia takwimu hizo kupanga bajeti za miaka inayofuata.
Amesema si kila chanzo cha mapato kinachopatikana katika mwaka mmoja kinaweza kuendelea kuwepo miaka inayofuata, akitoa mfano wa mapato yanayotokana na mauzo ya maeneo au ardhi ambayo yanaweza kuwa ya mara moja na hivyo kutokuwa na uhakika wa kujirudia.
Amesisitiza kuwa maafisa hao wana nafasi muhimu ya kutoa ushauri na kuwajengea uwezo viongozi pamoja na waandaaji wa bajeti katika halmashauri na sekretarieti za mikoa ili kuhakikisha mipango inayotayarishwa inaendana na hali halisi ya kifedha.
Aidha, amezitaka halmashauri kubaini na kuainisha makampuni na taasisi zote zinazopaswa kuchangia kupitia Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), hususan katika sekta ya madini na sekta nyingine, ili kuhakikisha zinachangia kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo iliyopo.
Amesema maafisa mipango na bajeti wanapaswa kuwa wabunifu katika kubaini taasisi mpya zinazostahili kutoa michango hiyo badala ya kutegemea makampuni yale yale kila mwaka, huku wakiweka mikakati ya kuwashirikisha wadau hao na kuhakikisha fedha za CSR zinapatikana na kutumika katika miradi ya maendeleo.
Hata hivyo amehimiza ushirikiano kati ya maafisa mipango, bajeti na viongozi wa halmashauri katika kutekeleza maelekezo hayo, akibainisha kuwa mafanikio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yanategemea maandalizi madhubuti na utekelezaji wa mipango kuanzia ngazi za Serikali za Mitaa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Serikali za Mitaa, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Angelista Kihaga, amesema Serikali imeendelea kuimarisha uwezo wa watumishi katika mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia mafunzo yanayolenga kuboresha uandaaji na usimamizi wa mipango na bajeti ili kuongeza ufanisi katika matumizi ya fedha za umma.
Kihaga ameeleza kuwa mafunzo hayo yanatoa fursa kwa washiriki kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto na kupata suluhisho zitakazosaidia kuimarisha ushirikiano kati ya idara na sekta mbalimbali katika halmashauri.
Naye Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Mipango na Uratibu Mkoa wa Dar es Salaam, Moses Chila, amesema mafunzo ya uandaaji na usimamizi wa mipango na bajeti yaliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI yamewajengea uwezo maafisa mipango, wachumi na maafisa bajeti katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi katika ngazi za mikoa na mamlaka za Serikali za Mitaa.
“Washiriki wamejipanga kuyatumia maarifa waliyopata kuboresha maandalizi ya bajeti ya mwaka wa fedha 2027/2028 na kuimarisha uwajibikaji katika utekelezaji wa shughuli za Serikali.”amesema Bw.Chila

















