MIKUMI
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesikiliza kero na maoni ya wananchi wa Jimbo la Mikumi na kutoa maelekezo ya kushughulikia changamoto mbalimbali, huku akichukua hatua za kutatua baadhi ya kero zilizowasilishwa na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Mji Mdogo wa Mikumi, mkoani Morogoro, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi.
Akijibu hoja za wananchi, Waziri Mkuu ameelekeza Bodi ya Sukari Tanzania kutuma wataalamu kukutana na wakulima wa miwa pamoja na vyama vya ushirika ili kubaini chanzo cha kushuka kwa bei ya zao hilo na kupata ufumbuzi. Kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji, amesema kikao cha mawaziri nane kitafanyika Novemba 29, 2026, kujadili taarifa ya timu iliyofanya uchunguzi na kuweka mikakati ya kutatua changamoto hiyo.
Aidha, amewataka wananchi kuheshimu mipango ya matumizi bora ya ardhi, kulinda vyanzo vya maji, kuepuka kujichukulia sheria mkononi na kuacha vitendo vya ukatili dhidi ya mifugo.
Akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa Jimbo la Mikumi ambaye pia ni Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Lazaro Londo amesema Jimbo la Mikumi ni eneo la kimkakati kutokana na shughuli za kilimo, biashara, utalii na usafirishaji na ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji uliofanyika katika sekta mbalimbali za maendeleo, ikiwemo elimu, afya, maji na miundombinu.
Amesema Serikali imeelekeza zaidi ya Shilingi bilioni 12 katika kuboresha elimu ya awali, msingi na sekondari, huku Jimbo la Mikumi likiwa na shule za sekondari za kidato cha tano na sita zaidi ya tano na kuongeza kuwa changamoto ya mabweni inaendelea kushughulikiwa ili kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Katika sekta ya afya, amesema zaidi ya Shilingi bilioni 12 zimeelekezwa kuboresha huduma, huku jimbo hilo likiwa na vituo vya afya zaidi ya sita ambapo kwa sekta ya maji , Mhe. Londo amesema zaidi ya Shilingi bilioni 21 zimetolewa kwa ajili ya kuboresha huduma hiyo, zikiwemo kilomita zaidi ya 66 za mabomba. Ameeleza kuwa licha ya uwekezaji huo, changamoto iliyopo ni kuwaunganisha wananchi na huduma ya maji ili wanufaike na miundombinu iliyowekwa.
Aidha, amesema Mikumi ni jimbo la kimkakati katika usafirishaji kutokana na malori yanayotoka Nyanda za Juu Kusini kupita katika eneo hilo. Ameeleza kuwa uboreshaji wa barabara ya Kilosa–Mikumi utarahisisha usafirishaji wa bidhaa na kupunguza muda wa safari kwa zaidi ya saa sita na kuishukuru Serikali kwa ukarabati unaoendelea kufanyika katika barabara hiyo na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza miundombinu inayounganisha maeneo ya uzalishaji na masoko.
Akizungumzia kilimo na viwanda, Mhe. Londo amesema kiwanda cha sukari cha Kilombero (Ilovo) kimechangia kuinua maisha ya wananchi wa Mikumi na kupambana na umasikini kupitia fursa za kiuchumi na ajira. Ameeleza kuwa uwekezaji wa zaidi ya Shilingi bilioni 300 umeelekezwa katika upanuzi wa kiwanda hicho. Hata hivyo, amesema wakulima wa miwa wanakabiliwa na changamoto ya kushuka kwa bei ya zao hilo, hivyo ameiomba Serikali kuingilia kati ili kupata suluhisho litakalowanufaisha wakulima na kuendeleza uzalishaji wa sukari nchini.
Ameongeza kuwa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya jimbo hilo, hivyo amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuiendeleza pamoja na miundombinu ya barabara zinazounganisha maeneo ya utalii, ikiwemo barabara ya Mbamba–Miyombo inayotarajiwa kufungua fursa zaidi za utalii na kuunganisha maeneo ya kiuchumi.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Queen Cuthbert Sendiga; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb.); Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji; Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Kaspar Mmuya; pamoja na Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Kundo A. Mathew.









