
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto katika Wizara ya Afya, Dkt. Ahmad Makuwani, amezipongeza taasisi za Serikali, zikiwemo Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wizara ya Maji na Wizara ya Ujenzi, kwa mchango wao katika kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto kupitia upatikanaji wa umeme, maji safi na miundombinu bora ya barabara nchini.

Akizungumza wakati wa kufungua semina ya wahariri wa vyombo vya habari iliyofanyika katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), jijini Dar es Salaam, Novemba 23, 2026, Dkt. Makuwani alisema huduma hizo zimeimarisha utoaji wa huduma za afya kwa kuwezesha upasuaji na matibabu ya dharura, kuzuia maambukizi na kurahisisha usafirishaji wa wagonjwa.
Alisema hadi mwaka 2024/2025, vijiji vyote 12,318, sawa na asilimia 100, vilikuwa vimeunganishwa na umeme, huku vijiji 10,779 vikiwa vimefikiwa na huduma ya maji safi, sawa na asilimia 83. Aidha, mtandao wa barabara zinazopitika wakati wote wenye urefu wa kilometa 144,300 umechangia kurahisisha huduma za rufaa.
Dkt. Makuwani alisema mafanikio hayo yanaenda sambamba na utekelezaji wa mikataba miwili ya uwajibikaji iliyoanzishwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwemo Kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama iliyoanzishwa mwaka 2018 na mkataba wa kuimarisha lishe ulioingiwa mwaka 2022. Aliongeza kuwa bajeti ya sekta ya afya imeongezeka kutoka Shilingi trilioni 2.46 mwaka 2023/2024 hadi trilioni 3.7 mwaka 2026/2027.
Alisema Serikali imeongeza zahanati kutoka 4,127 hadi 6,589, vituo vya afya kutoka 535 hadi 1,067 na hospitali za wilaya kutoka 77 hadi 194 kati ya mwaka 2015/2016 na 2024/2025. Pia, magari ya kubebea wagonjwa yameongezeka kutoka 540 mwaka 2021 hadi 1,113 mwaka 2026, huku mfumo wa rufaa wa kielektroniki wa m-Mama ukiwa umewezesha kusafirisha wagonjwa 250,000 hadi Agosti 2026.
Akizungumzia huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto, alisema wajawazito wanaohudhuria kliniki kwa mara ya kwanza wameongezeka kutoka asilimia 84 mwaka 2022 hadi asilimia 86, huku wanaohudhuria kliniki angalau mara nne wakiongezeka kutoka asilimia 65 hadi asilimia 81. Vilevile, wajawazito wanaojifungulia katika vituo vya afya wameongezeka kutoka asilimia 81 hadi asilimia 85.
Dkt. Makuwani alisema mafanikio hayo yamechangia kupungua kwa vifo vitokanavyo na uzazi kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2016 hadi 104 mwaka 2022, huku vifo vya watoto vikishuka kutoka 67 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1,000. Alisema Serikali inalenga kufikia mwaka 2030 kupunguza vifo vya uzazi hadi chini ya 70 kwa kila vizazi hai 100,000 na vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano hadi chini ya 25 kwa kila vizazi hai 1,000.
Alifafanua kuwa mkutano wa tatu wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto pamoja na Lishe, utakaofanyika Novemba 25 hadi 27, 2026, umeandaliwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na OWM-TAMISEMI na wadau wa maendeleo. Rais Samia anatarajiwa kuwa mgeni rasmi, kufungua mkutano huo, kusaini mkataba wa pili wa uwajibikaji kwa wakuu wa mikoa na kuzindua ripoti ya hali ya vifo vitokanavyo na uzazi na watoto nchini. Dkt. Makuwani amevitaka vyombo vya habari kuelimisha jamii kuhusu afya ya uzazi, mama na mtoto na kuhamasisha wananchi kujiunga na bima ya afya.










