
KENYA :Waziri wa Ujenzi, Masanja Kungu Kadogosa, amesema Serikali ya Tanzania imejipanga kuimarisha utekelezaji wa miradi ya miundombinu kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public Private Partnership – PPP), kwa kujifunza uzoefu wa Kenya katika kuvutia uwekezaji na kusimamia miradi mikubwa ya maendeleo.
Kadogosa ameyasema hayo jijini Nairobi, Kenya, wakati wa Kongamano la 16 la Bara la Afrika kuhusu Ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), ambapo amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kutumia mfumo huo kama njia mojawapo ya kuongeza uwezo wa kugharamia na kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu.
Amesema Tanzania inaendelea kuandaa na kutekeleza mikakati ya kutumia mfumo wa PPP katika miradi mbalimbali, hivyo kujifunza uzoefu wa Kenya kutasaidia kubaini mifumo bora ya utekelezaji, namna ya kuvutia wawekezaji binafsi na kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Aidha, amesema katika mazungumzo yaliyofanyika pembezoni mwa kongamano hilo, wamejadili fursa za uwekezaji katika sekta ya miundombinu nchini Tanzania, hususan miradi ya barabara ya Kibaha–Chalinze, Chalinze–Morogoro, Morogoro–Iringa na Igawa–Tunduma.
Kadogosa ameeleza kuwa miongoni mwa mambo muhimu yaliyojadiliwa ni namna Kenya ilivyoanzisha Mfuko wa Taifa wa Miundombinu (Kenya National Infrastructure Fund), wenye mtaji unaokadiriwa kufikia dola za Marekani bilioni tatu, kwa lengo la kusaidia kugharamia miradi ya miundombinu na kupunguza vihatarishi vya uwekezaji vinavyoweza kuwafanya wawekezaji binafsi kusita kushiriki katika miradi ya PPP.
Amesisitiza kuwa uzoefu huo ni muhimu kwa Tanzania katika kuimarisha mazingira ya uwekezaji, kuongeza ushiriki wa sekta binafsi na kuhakikisha miradi mikubwa ya miundombinu inapata vyanzo endelevu vya fedha kwa ajili ya utekelezaji wake.
Kongamano hilo limewakutanisha wadau kutoka mataifa mbalimbali, yakiwemo Kenya, Uganda, Ufaransa, Tunisia, Ivory Coast na Senegal, kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujadili mikakati ya kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika kufadhili na kutekeleza miradi ya maendeleo barani Afrika.
Hatua hiyo inaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi shindani na jumuishi kupitia uwekezaji katika miundombinu ya kisasa, kuongeza ushiriki wa sekta binafsi na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati kwa maendeleo ya Taifa.









