Home Kitaifa DCEA, Kenya wavunja mtandao wa Kimataifa wa dawa za kulevya , watuhumiwa...

DCEA, Kenya wavunja mtandao wa Kimataifa wa dawa za kulevya , watuhumiwa 7 mbaroni

Celebrating 25 Years of NHIF
  • Paketi 753 za heroin na methamphetamine zakamatwa Tanzania na Kenya
  • Watuhumiwa wanadaiwa kuendesha biashara hiyo katika nchi kadhaa, ikiwemo Afghanistan na Afrika Kusini
  • Magari mawili yaliyotumika kusafirisha dawa hizo nayo yakamatwa

Na Esther Mnyika, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Kitengo cha Kitaifa cha Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini Kenya (NANB), imefanikiwa kuvunja sehemu ya mtandao wa kimataifa wa biashara ya dawa za kulevya baada ya kukamata paketi 753 za dawa hizo katika operesheni za pamoja zilizofanyika Tanzania na Kenya, huku watuhumiwa saba wakitiwa mbaroni.

FAHARI AFYA

Operesheni hizo, zilizofanyika Novemba 6 na 7, 2026, zimewezesha kukamatwa kwa paketi 299 za heroin na methamphetamine jijini Dar es Salaam, pamoja na paketi nyingine 454 za methamphetamine nchini Kenya.

Akizungumza Novemba, 9 2026 jijini Dar es Salaam kuhusu mafanikio hayo, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema katika operesheni ya kwanza iliyofanyika Novemba 6, 2026, eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam, jumla ya paketi 299 zilikamatwa, zikiwemo paketi 24 za heroin na 275 za methamphetamine.

“Dawa hizi zilikutwa zimefichwa ndani ya magari mawili aina ya Ford Ranger yenye namba za usajili T.950 ERA na T.417 EJZ, ambayo yamekamatwa na kushikiliwa kwa tuhuma za kutumika katika kusafirisha dawa hizi,“amesema.

Katika operesheni hiyo, watuhumiwa wanne walikamatwa. Wao ni Juma Slaati Kisomeko (36), raia wa Uganda, pamoja na Watanzania Issa Said Nassoro (34), Ibrahim Said Chembela (30) na Mohamed Ally Shemtuu (45).

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na watuhumiwa, dawa hizo zilichukuliwa Mombasa nchini Kenya na kusafirishwa kuingia Tanzania kupitia mpaka wa Horohoro, mkoani Tanga.

Lyimo amesema taarifa hizo ziliiwezesha DCEA kuwasiliana na mamlaka za Kenya, hatua iliyofungua ukurasa mpya wa operesheni za pamoja zilizolenga kubaini chanzo cha dawa hizo, maeneo yaliyotumika kuzihifadhi na kuwafichua wahusika wengine wa mtandao huo.

Ushirikiano huo ulizaa matokeo siku iliyofuata, Novemba 7, 2026, baada ya maafisa wa DCEA na NANB kufanya operesheni katika eneo la Kwale, Mombasa nchini Kenya, na kukamata paketi nyingine 454 za methamphetamine pamoja na kuwakamata watuhumiwa watatu.

Watuhumiwa hao ni Saleh Khamis Baseleman (45), maarufu Mbwiga, na Seif Said Hamad (54), anayefahamika kwa jina la Babu Seif, wote raia wa Tanzania, pamoja na Zuraicah Ahmed Hussein (25), raia wa Uganda.

Kwa mujibu wa Lyimo, baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa wanadaiwa kuwa miongoni mwa vinara wa mtandao wa kimataifa unaojihusisha na ununuzi, usafirishaji na usambazaji wa dawa za kulevya katika nchi mbalimbali.

Amezitaja nchi zinazodaiwa kuhusishwa na mtandao huo kuwa ni Afghanistan, Afrika Kusini, Msumbiji, Zambia, Malawi, Uganda, Kenya, Tanzania na Dubai.

Amesema miongoni mwa wanaodaiwa kuwa na nafasi kubwa katika mtandao huo ni Saleh Khamis Baseleman, maarufu Mbwiga, ambaye anadaiwa kununua dawa za kulevya moja kwa moja kutoka Afghanistan na kuzisafirisha kwa njia ya bahari hadi katika fukwe za Mombasa nchini Kenya, kabla ya kusambazwa katika nchi mbalimbali, ikiwemo Tanzania.

Aidha, Mbwiga anahusishwa na ukamataji wa tani 3.5 za dawa za kulevya uliofanywa na DCEA mwezi Desemba 2023 katika maeneo ya Kigamboni jijini Dar es Salaam na mkoani Iringa.

Kwa sasa, taratibu za kisheria na ushirikiano baina ya mamlaka za Tanzania na Kenya zinaendelea kwa lengo la kuhakikisha watuhumiwa wote wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Katika hatua nyingine, Kamishna Jenerali Lyimo amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanahitaji ushirikiano wa karibu katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa, kutokana na biashara hiyo kuvuka mipaka ya nchi.

Amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na mamlaka husika kwa kutoa taarifa kuhusu viashiria vya biashara na matumizi ya dawa za kulevya ili kusaidia kudhibiti uhalifu huo na kulinda usalama wa jamii.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!