
Jamii na wadau mbalimbali wametakiwa kushirikiana katika kuhakikisha mtoto wa kike anapata mahitaji muhimu ya kujisitiri wakati wa hedhi, ili kuepusha changamoto zinazoweza kumfanya akose masomo au kukatiza ndoto zake za kielimu.
Wito huo umetolewa wakati wa harambee maalumu ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ununuzi wa taulo za kike zitakazotolewa kwa wanafunzi 5,000 wa shule za msingi na sekondari kutoka familia zenye changamoto za kiuchumi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Lorna Dadi Foundation, Lorna Dadi, amesema ni muhimu jamii kushiriki katika kutatua changamoto zinazowakabili wasichana, hususan wale wanaotoka katika familia zenye kipato cha chini.
Kupitia mradi wa Nisitiri, taasisi hiyo inalenga kuwawezesha wanafunzi wa kike kupata taulo za kujisitiri na kuendelea na masomo yao bila vikwazo vinavyotokana na changamoto za hedhi.
Hatua hiyo imeenda sambamba na uzinduzi wa kitabu maalumu, ambacho mapato yatakayopatikana yatasaidia kugharamia ununuzi wa taulo hizo, huku kikilenga pia kuongeza uelewa kuhusu changamoto za hedhi na umuhimu wa kumlinda mtoto wa kike.









