Na Mwandishi Wetu.
KAMATI ya Kanuni na Sheria Ndogo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar imepongeza uwekezaji uliofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika maabara za Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ikisema umeimarisha uwezo wa upimaji, ugezi na usahihi wa vipimo nchini.
Pongezi hizo zimetolewa leo Oktoba 19, 2026 na na Kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Hudhaima Mbaraka Tariq, ilipotembelea Ofisi za TBS Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujifunza kuhusu utekelezaji wa kanuni za ugezi na namna shirika hilo linavyosimamia usahihi wa vipimo na ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Mhe. Hudhaima amesema ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwa kamati hiyo, kutokana na fursa waliyoipata ya kujionea vifaa vya kisasa na kujifunza uzoefu wa TBS katika kusimamia masuala ya ugezi.
“Tumekuja kujifunza kuhusu masuala ya ugezi ambayo tunayapitia katika kanuni zetu. Tumeona uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika vifaa vya kisasa na namna unavyosaidia kuhakikisha usahihi wa vipimo, mizani na huduma nyingine,” amesema.
Ameongeza kuwa kamati hiyo itatumia uzoefu iliyoupata kutoka TBS kupitia mchakato wa kupitia kanuni husika na kuboresha maeneo yatakayohitaji maboresho kwa manufaa ya wananchi.
Aidha, amesema ushirikiano uliopo kati ya TBS na taasisi za Zanzibar, ikiwemo Shirika la Viwango Zanzibar (ZBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA), ni muhimu katika kuimarisha usimamizi wa ubora na usalama wa bidhaa katika pande zote mbili za Muungano.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Sempeho Manongi, amesema Serikali inathamini ziara hiyo na kuamini kuwa uzoefu watakaobadilishana kati ya TBS na ZBS utasaidia kuimarisha mifumo ya viwango kwa manufaa ya Serikali zote mbili na wananchi kwa ujumla.
Manongi amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya viwango ili kulinda afya za wananchi, kuongeza ubora wa bidhaa na kukuza ushindani katika soko, hatua itakayochangia maendeleo ya sekta ya viwanda na biashara nchini.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi, amesema shirika hilo limefurahi kupokea kamati hiyo kwa kuwa ziara hiyo ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano wa kitaasisi na kubadilishana uzoefu katika usimamizi wa viwango na utekelezaji wa sheria na kanuni.
Amesema TBS inaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia ZBS, ZFDA na taasisi nyingine husika, kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa, kuingizwa na kuuzwa katika pande zote mbili zinakidhi viwango vya ubora na usalama.
Dkt. Ashura amesema wajumbe wa kamati hiyo pia walipata fursa ya kutembelea maabara za TBS na kujionea uwekezaji uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Ameeleza kuwa TBS ina maabara 10 za upimaji na maabara sita za ugezi, ambazo zina uwezo wa kutoa huduma kwa kuzingatia umahiri wa kimataifa, hatua inayosaidia kuhakikisha usahihi wa vipimo na kuaminika kwa matokeo yanayotolewa.
Amesisitiza kuwa TBS itaendelea kuwa taasisi wezeshi kwa wafanyabiashara, wananchi na Serikali kwa ujumla, kwa kuhakikisha bidhaa na huduma zinakidhi matakwa ya viwango, huku ikichangia kukuza sekta ya viwanda na biashara na kulinda afya na usalama wa wananchi.









