
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Denis Londo (Mb), amesema Serikali itaendelea kuhimiza matumizi ya teknolojia mahali pa kazi ili kuboresha utekelezaji na utendaji wa kazi.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Dennis Londo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa baraza la wafanyakazi wa BRELA uliofanyika mkoani leo mkoani Morogoro na kuipongeza wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa hatua ilizochukua kuboresha Mfumo wa Huduma kwa Njia ya Mtandao (BRELA Online Services – BOS).

Amesema matumizi hayo ya teknolojia yatasaidia kuboresha utendaji kazi sambamba na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.
“Nimefurahishwa na hatua za BRELA katika kuboresha Mfumo wa BRELA Online Services (BOS), ambapo moduli tano kati ya saba zimeanza kutumika na ninawasisitiza kuendelea kuongeza ufanisi, kupunguza muda wa utoaji huduma na kuboresha huduma kwa wananchi na wafanyabiashara,” alisema Mhe. Londo.
Aidha, ameitaka BRELA kuendelea kufanya mapitio na maboresho ya sheria na kanuni mbalimbali kwa kushirikiana na wadau, kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara na kurahisisha utoaji wa huduma nchini na kuongeza kuwa mchakato huo unapaswa kuwashirikisha wadau kikamilifu ili kupunguza urasimu, kuondoa masharti yanayokwamisha shughuli za biashara na kuimarisha uzingatiaji wa sheria.

Kwa upande wake Bw. Elias Kalist, akimwakilisha Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara BRELA, amesema Bodi inatambua na kuthamini jitihada zinazofanywa na taasisi katika kuimarisha matumizi ya teknolojia na kuboresha utoaji wa huduma.
“Bodi ya Ushauri inaendelea kusisitiza umuhimu wa BRELA kutumia mifumo ya kidijitali, kuongeza uwajibikaji na kuhakikisha Wakala inachangia kikamilifu katika utekelezaji wa mipango ya Serikali ya kukuza sekta binafsi na uwekezaji,” amesema Bw. Kalist.

Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, akiwasilisha hotuba yake, amesema katika Mwaka wa Fedha 2026/2027, Wakala utaendelea kuelekeza nguvu katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa BRELA wa mwaka 2026/2027–2030/2031, kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali na mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema maeneo yatakayopewa kipaumbele ni pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma kupitia mifumo ya kielektroniki, kukamilisha maboresho ya BOS, kuwezesha utoaji wa leseni za biashara za Kundi B kwa kushirikiana na mamlaka husika, pamoja na kuendelea kupitia sheria na kanuni mbalimbali kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa BRELA kimefanyika kwa siku tatu, kuanzia Oktoba 10 hadi 12, 2026, mkoani Morogoro. Kikao hicho kimehusisha mafunzo kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, msongo wa mawazo na afya ya akili, pamoja na mafao, haki na wajibu wa wanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), kwa lengo la kuongeza uelewa wa watumishi kuhusu afya, ustawi na maandalizi ya maisha ya baadaye.









