
SERIKALI inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha taaluma na hadhi ya walimu nchini, ikiwamo kuanzisha mafunzo ya vitendo kwa wahitimu wa ualimu kabla ya kuajiriwa, pamoja na kuanzisha mfumo wa utoaji leseni kwa walimu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ameyasema hayo leo, Oktoba 5, 2026, wakati akitoa salamu za Siku ya Mwalimu Duniani katika Taasisi ya Uongozi wa Elimu (ADEM), Bagamoyo.
Prof. Mkenda amesema Serikali kupitia Bodi ya Kitaaluma ya Walimu (Teachers Profession Board) imejipanga kutoa leseni kwa walimu wote, utaratibu ambao utatangazwa, huku leseni hizo zikitarajiwa kuwawezesha walimu kupata fursa za ajira ndani na nje ya Tanzania.
Amesema Bodi hiyo pia itasimamia mafunzo ya vitendo kwa walimu kabla ya ajira (internship), ambapo Serikali tayari imetenga fedha kwa wanafunzi wote wanaosoma ualimu ngazi ya Diploma wanaotarajiwa kuhitimu katika mwaka wa fedha 2026/27.
Aidha, wahitimu hao watakapomaliza masomo yao watapelekwa katika shule mbalimbali za Serikali kwa ajili ya kupata uzoefu wa vitendo, huku Serikali ikigharamia fedha za kujikimu wakati wa mafunzo hayo.
Amesema utaratibu huo pia utaendelea kutolewa kwa wahitimu wa vyuo vikuu wenye Shahada za Ualimu, hatua ambayo inalenga kuimarisha taaluma ya walimu kabla ya kuingia rasmi katika ajira.
Pamoja na hayo amesema Serikali pia inaendelea kupanga upya Vyuo vya Ualimu ili majukumu yake yaendane na mahitaji ya sasa ya elimu na kuongeza uwezo wa wahitimu.
Amesema baadhi ya Vyuo vya Ualimu vitaandaliwa kutoa mafunzo ya ufundi, akitolea mfano Chuo cha Ualimu Mtwara, ambacho kinatarajiwa kutoa Diploma katika elimu ya ufundi, michezo na maeneo mengine.
Prof. Mkenda amesema, mfumo huo utawapa wahitimu fursa pana zaidi za ajira kwani wanaweza kufanya kazi kama walimu au kutumia taaluma zao katika sekta nyingine.
Hata hivyo Waziri Mkenda amesema walimu wana nafasi kubwa katika utekelezaji wa mageuzi yanayoendelea katika sekta ya elimu nchini, akisisitiza kuwa Serikali inatambua mchango wao katika malezi na ujenzi wa Taifa.
Amesema Tanzania inaelekea katika utekelezaji wa elimu ya lazima hadi kidato cha nne, ambapo elimu ya msingi itakuwa ya miaka 10, kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne.
Amesema kwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mikoa inapaswa kujiandaa kuhakikisha ifikapo mwaka 2028 wanafunzi wanaohitimu darasa la sita na wale watakaohitimu darasa la saba mwaka 2027 wanaendelea na elimu hadi kidato cha nne.
Prof. Mkenda amesema utekelezaji wa mpango huo unahitaji maandalizi makubwa ya miundombinu ya shule za sekondari, huku Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI ikiendelea na maandalizi ya kuongeza madarasa na kujenga shule mpya.
Amesema lengo ni kuhakikisha watoto wanaopaswa kuendelea na kidato cha kwanza wanapata nafasi katika shule za sekondari, ikiwamo kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na shule ya sekondari.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Maulid J. Maulid, amesema taasisi hiyo inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia mageuzi yanayoendelea katika sekta ya elimu, mabadiliko ya Sera ya Elimu na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema ADEM inaendelea kutoa mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa elimu nchini, huku maboresho ya miundombinu yakiendelea katika taasisi hiyo.
Amesema miongoni mwa miradi inayoendelea ni ujenzi wa jengo la utawala pamoja na kumbi za mihadhara na mikutano, inayofadhiliwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa hatua zinazochukuliwa kuboresha sekta hiyo, akisema Wilaya ya Bagamoyo imejiandaa kuongeza na kuboresha miundombinu ya shule za sekondari.
Amesema baadhi ya shule mpya tayari zimeanza kujengwa na uongozi wa wilaya utaendelea kusimamia miradi hiyo ili ikamilike kwa wakati.









