
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Uislamu unahimiza upendo, amani, umoja na mshikamano, misingi muhimu katika kujenga jamii yenye utulivu, maelewano na maendeleo.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 4 Oktoba 2026, katika Muhadhara wa Kiislamu ulioandaliwa na Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar na kufanyika Masjid Jamiu Zinjibar, Mazizini, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amewataka waumini kuzingatia mafundisho ya Qur’ani Tukufu na Mtume Muhammad (S.A.W.), kuheshimiana, kusaidiana, kusameheana na kudumisha amani, huku wakijiepusha na mambo yanayoleta chuki na migawanyiko.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza Ofisi ya Mufti Mkuu kwa juhudi za kuendeleza elimu ya dini na kuimarisha amani, upendo na mshikamano katika jamii.
Muhadhara huo umehudhuriwa na viongozi na wananchi mbalimbali, pamoja na Masheikh kutoka ndani na nje ya nchi, akiwemo Mufti Ismail Menk kutoka Zimbabwe.









