Home Biashara UTURUKI KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KUONGEZA THAMANI YA BIDHAA -LONDO

UTURUKI KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KUONGEZA THAMANI YA BIDHAA -LONDO

📌Afanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Viwanda na Teknolojia wa Uturuki;

📌Ashiriki tamasha la 15 la Anga na Teknolojia nchini Uturuki

📌Tanzania yapewa kipaumbele kushirikiana na Uturuki kwenye Viwanda na kuongeza thaman

Uturuki

Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi zitakazopewa kipaumbele katika mpango mpya wa Uturuki wa kushirikiana na nchi zinazoendelea katika ujenzi wa viwanda, kuongeza thamani ya bidhaa na kuunganisha viwanda, huku wataalamu wa nchi hizo wakitarajiwa kubaini maeneo ya kimkakati ya kuanza utekelezaji wa ushirikiano huo.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, Oktoba 1, 2026 nchini Uturuki, katika Tamasha la 15 la Anga na Teknolojia (TEKNOFEST) 2026, ambapo amesema amefanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Viwanda na Teknolojia wa Uturuki, Muhammet Kasım Gönüllü, kuhusu namna nchi hizo zinavyoweza kushirikiana katika kuendeleza sekta ya viwanda na matumizi ya teknolojia katika uzalishaji.

Londo amesema mpango huo, ambao umeanzishwa na Uturuki mwezi huu, unalenga kushirikisha sekta binafsi, taasisi za fedha, waendeshaji wa teknolojia na viwanda kutoka pande zote mbili, huku Tanzania ikitarajiwa kuwa nchi ya majaribio katika utekelezaji wa mpango huo.

Katika eneo la kilimo na mifugo, Londo amesema Tanzania imejadili uwezekano wa kubadilishana uzoefu kupitia programu ya Uturuki inayofahamika kama TUME, ambayo amesema ina mfanano na mpango wa Tanzania wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT).

Aidha, amesema Tanzania na Uturuki zimejadili ushirikiano katika mabadiliko ya kidijitali, sayansi na teknolojia, biashara mtandao na serikali mtandao, huku hatua hiyo ikiendana na mwelekeo wa Tanzania katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Katika mazungumzo hayo, Londo pia amekutana na Savaş Yanık, Naibu Meneja Mkuu wa HAVELSAN anayesimamia Teknolojia za Amri, Udhibiti na Ulinzi, kwa ajili ya kujadili fursa za ushirikiano katika matumizi ya teknolojia na mifumo ya kisasa.

HAVELSAN ni kampuni ya teknolojia ya Uturuki inayojihusisha na mifumo ya ulinzi, teknolojia za kidijitali, uigaji na mafunzo pamoja na mifumo ya amri na udhibiti.

Londo amesema mazungumzo hayo yanafungua fursa kwa Tanzania kuendelea kujifunza na kutumia uzoefu wa Uturuki katika teknolojia, viwanda na ubunifu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uzalishaji, thamani ya bidhaa na matumizi ya teknolojia katika uchumi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!