Na Mwandishi Wetu.
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kuimarisha juhudi zake za kuwafikia wananchi kwa kutoa elimu kuhusu viwango, ubora na usalama wa bidhaa kupitia ushiriki wake katika Tamasha la Kariakoo (Kariakoo Festival), lililofanyika katika Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Katika tamasha hilo lililoanza Septemba 25 na kuhitimishwa leo, Septemba 27, 2026, TBS imetumia banda lake kutoa elimu kwa wananchi waliotembelea tamasha hilo, kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango na kuhakikisha bidhaa zinazotumika zinakidhi matakwa ya ubora na usalama.
Afisa Udhibiti Ubora wa TBS, Bw. Kelvin Mtebene, alikuwa miongoni mwa wataalamu waliotoa elimu hiyo kwa wananchi, akieleza masuala mbalimbali yanayohusu viwango na umuhimu wa kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa, kuuzwa na kutumiwa zinazingatia matakwa ya ubora na usalama.
Kupitia elimu hiyo, wananchi wamepata fursa ya kufahamu namna ya kutambua na kuchagua bidhaa zinazokidhi viwango, hatua inayosaidia kulinda afya na usalama wao pamoja na kuwajengea uwezo wa kufanya maamuzi sahihi wanapofanya manunuzi.

Ushiriki wa TBS katika tamasha hilo pia umekuwa fursa muhimu ya kulisogeza Shirika karibu zaidi na wananchi, kwa kuwapa nafasi ya kuuliza maswali, kupata ufafanuzi na kutoa maoni kuhusu huduma zinazotolewa na TBS, hususan katika eneo la udhibiti wa ubora wa bidhaa nchini.
Kupitia mazungumzo ya ana kwa ana na wananchi, TBS imeendelea kutekeleza jukumu lake la kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa viwango na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu wajibu wa kila mdau katika kuhakikisha bidhaa zinazotumika katika jamii zinakuwa na ubora unaotakiwa.
Aidha, uwepo wa TBS katika Tamasha la Kariakoo unaonesha umuhimu wa kutumia majukwaa ya kijamii na kibiashara kuwafikia wananchi wengi zaidi, wakiwemo wafanyabiashara na watumiaji wa bidhaa, ili kuongeza uelewa kuhusu masuala ya viwango na kuhamasisha matumizi ya bidhaa bora na salama.









