Home Kitaifa TMDA YAWANOA WATAALAM WA AFYA KIBAHA KUHUSU DAWA TIBA ZENYE ASILI YA...

TMDA YAWANOA WATAALAM WA AFYA KIBAHA KUHUSU DAWA TIBA ZENYE ASILI YA KULEVYA

Na Mwandishi Wetu, Kibaha.

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Mashariki, kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na Bohari ya Dawa (MSD), imetoa mafunzo maalum kwa Waganga Wafawidhi, Wafamasia, Wauguzi na Wakaguzi wa dawa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha na Manispaa ya Kibaha Mjini, September 18, 2026.

Mafunzo hayo yamelenga kudhibiti matumizi holela ya dawa kama Pethidine, Morphine, Diazepam (Valium) na Tramadol, ambazo hutumika kutuliza maumivu makali ya saratani na upasuaji, lakini zikitumika vibaya huleta uraibu.

Akifungua mafunzo hayo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dk. Kusirye Ukio, amewataka washiriki kuzingatia maadili ya taaluma na kusimamia viapo vyao kwa kuwa usalama wa jamii uko mikononi mwao.

Kaimu Meneja wa TMDA Kanda ya Mashariki, Keddy Manga, amesema mafunzo hayo ni mkakati wa Serikali kuhakikisha dawa hizo muhimu kwa wagonjwa haziingii mitaani kinyume cha sheria.

“Jukumu la msingi la TMDA ni kuhakikisha dawa, vifaa tiba na vitendanishi ni bora, salama na vyenye ufanisi. Dawa hizi za maumivu makali zisipotumika kwa kufuata miongozo zinaweza kusababisha uraibu,” amesema Manga.

Mfamasia kutoka MSD, Suzana Majule, amesema wataendelea kutoa elimu ya jinsi ya kuomba, kupata na kuhifadhi dawa hizo vituoni, huku akisisitiza kuwa usambazaji wake lazima uambatane na kibali kutoka TMDA.

Naye Mwakilishi wa DCEA, Mfamasia Upendo Chenya, amesema nchi imeshuhudia ongezeko la matumizi mabaya ya dawa hizo kama mbadala wa dawa za kulevya.

Amesema DCEA na TMDA wameanza na Kibaha lakini wataendelea na maeneo mengine ya Pwani ikiwemo Bagamoyo.

“Matumizi ya dawa za kulevya kwa kawaida huanzia na dawa tiba zenye asili ya kulevya kutokana na upatikanaji wake rahisi vituo vya afya na famasi. Wasimamizi wa vituo na wafamasia wanapaswa kuzisimamia kikamilifu ili zisifike kwa watu wasio stahili,” amesema Chenya.

Ameongeza kuwa DCEA itaendelea kudhibiti utoaji wa dawa za jamii ya saikotropiki na narkotiki kwa kuhakikisha zinatolewa kwa cheti halali cha daktari.

Kwa upande wao, wataalamu wa afya waliohudhuria mafunzo hayo wameahidi kuzingatia maelekezo na kutoa dawa hizo kwa cheti halali pekee.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!