Home Kitaifa COASCO: UKAGUZI WA VYAMA VYA USHIRIKA NI NGUZO YA KUIMARISHA KILIMO NA...

COASCO: UKAGUZI WA VYAMA VYA USHIRIKA NI NGUZO YA KUIMARISHA KILIMO NA UCHUMI WA TAIFA

Magrethy Katengu–Dar es Salaam:

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), Jeremiah Mugeta, amesema sekta ya kilimo na ushirika zinaendelea kuwa nguzo muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania, huku akisisitiza kuwa ukaguzi wa mara kwa mara wa vyama vya ushirika unalenga kuongeza uwazi, uwajibikaji na imani kwa wanachama.

Akizungumza baada ya kutembelea banda la Wizara ya Kilimo katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mgeta alisema ameridhishwa na kazi kubwa inayofanywa na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo katika kuendeleza sekta ya kilimo kupitia utoaji wa huduma, elimu na ubunifu mbalimbali.

Alisema takwimu zinaonyesha kuwa sekta ya kilimo inachangia zaidi ya asilimia 26 ya Pato la Taifa (GDP), huku mazao yanayozalishwa kupitia mfumo wa ushirika yakichangia zaidi ya dola bilioni mbili za Marekani kwa mwaka, jambo linalodhihirisha nafasi kubwa ya ushirika katika maendeleo ya uchumi wa nchi.

Mugeta alisema COASCO imejipanga kuhakikisha vyama vya ushirika vinaendelea kuwa imara kwa kufanya ukaguzi wa kitaalamu, kutoa elimu kwa wanachama na viongozi wa ushirika, pamoja na kusimamia uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa vyama hivyo.

Alieleza kuwa shirika hilo litatoa ripoti ya ukaguzi wa mwaka wa fedha 2025/2026 mwezi Septemba mwaka huu, ili kuwapa wananchi, wanachama na wadau wa ushirika taarifa kuhusu hali halisi ya vyama vya ushirika nchini na mapendekezo ya kuboresha utendaji wake.

Aidha, alisema kuanzia Julai 20, mwaka huu, COASCO itaanza rasmi awamu ya kwanza ya ukaguzi wa vyama vya ushirika kwa mwaka wa fedha 2026/2027, huku akivitaka vyama vyote kuandaa na kuwasilisha kwa wakati taarifa zao za fedha katika ofisi za COASCO zilizopo karibu mikoa yote ya Tanzania Bara.

Mugeta alisema tayari kumekuwa na maboresho makubwa katika utendaji wa vyama vya ushirika, akibainisha kuwa idadi ya vyama vinavyopata hati safi za ukaguzi imeongezeka kutoka takribani asilimia nne katika miaka ya nyuma hadi kufikia zaidi ya asilimia 16 kwa sasa, huku idadi ya hati zenye maoni ikipungua kwa kiwango kikubwa.

Alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali chini ya uongozi wa kwa kuendelea kuimarisha sekta ya ushirika kupitia uwekezaji katika vifaa vya kazi na mazingira bora ya utekelezaji wa majukumu ya ukaguzi. Pia alimpongeza kwa juhudi za kuendeleza sekta ya kilimo na ushirika.

Mugeta amesisitiza kuwa COASCO itaendelea kutekeleza wajibu wake kwa uadilifu na weledi ili kuhakikisha vyama vya ushirika vinakuwa imara, vinazingatia misingi ya utawala bora na vinachangia kikamilifu maendeleo ya wakulima pamoja na uchumi wa Taifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!