Home Kitaifa WANANCHI WAASWA KUWA MAKINI DHIDI YA BIDHAA BANDIA SOKONI

WANANCHI WAASWA KUWA MAKINI DHIDI YA BIDHAA BANDIA SOKONI

Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) imeendelea kuimarisha kampeni ya utoaji elimu kwa umma kuhusu madhara ya biashara ya bidhaa bandia, ikisisitiza kuwa utengenezaji, usambazaji na uuzaji wa bidhaa hizo ni kosa la jinai linaloadhibiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Akizungumza leo Juni 22, 2026, katika eneo la Kariakoo Jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa FCC, Bi. Roberta Feruzi, amesema bidhaa bandia zina athari kubwa kwa uchumi, afya na usalama wa wananchi, huku zikidhoofisha ushindani wa haki katika biashara.

Amesema watu watakaobainika kujihusisha na biashara ya bidhaa bandia wanaweza kukabiliwa na adhabu ya kifungo cha kati ya miaka minne hadi 15 jela pamoja na faini inayofikia kati ya Shilingi milioni 10 na milioni 50, kulingana na masharti ya sheria husika.

Bi. Feruzi ameeleza kuwa FCC inaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za ndani na kimataifa katika kudhibiti bidhaa bandia ili kuhakikisha haziingii nchini, hazisambazwi katika soko la ndani, wala kutumiwa kama njia ya kupitishwa kwenda mataifa mengine kupitia mifumo ya usafirishaji.

Amebainisha kuwa nafasi ya Tanzania kama lango muhimu la biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki inaifanya nchi kuwa miongoni mwa maeneo yanayoweza kutumiwa na wahalifu kusafirisha bidhaa bandia, hali inayohitaji ushirikiano wa karibu kati ya serikali, sekta binafsi na wananchi katika kupambana na tatizo hilo.

Kwa mujibu wa Bi. Feruzi, biashara ya bidhaa bandia si changamoto ya Tanzania pekee, bali ni tatizo la kimataifa linalosababishwa na watu wasio waaminifu wanaotafuta faida kwa kutumia kazi, ubunifu na alama za biashara za wengine kinyume cha sheria.

Ametoa wito kwa wananchi na wafanyabiashara kuwa makini wanaponunua au kuuza bidhaa, huku akiwahimiza kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapobaini uwepo wa bidhaa zinazohisiwa kuwa bandia.

Vilevile, amesema Tanzania itaadhimisha Siku ya Kitaifa ya Udhibiti wa Bidhaa Bandia Juni 25, 2026, yakiwa na  kauli mbiu isemayo: “Linda Maisha na Masoko Dhidi ya Pombe, Vilainishi na Sigara Bandia” ambapo maadhimisho hayo yatatumika kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu athari za bidhaa bandia na kuimarisha juhudi za kitaifa na kimataifa za kupambana na biashara hiyo haramu.

Amesisitiza kuwa mafanikio ya vita dhidi ya bidhaa bandia yanategemea ushirikiano wa wadau wote, ikiwemo Serikali, wafanyabiashara , wazalishaji na wananchi, ili kulinda uchumi wa taifa, afya za watumiaji na mazingira ya biashara yenye ushindani wa haki.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!