
Afisa wa Idara ya Masoko wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Antonia James Masoy, amewahimiza wajasiriamali kupata mafunzo rasmi yanayotolewa na SIDO kabla ya kuwasilisha bidhaa zao katika Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ili kuongeza uwezekano wa bidhaa hizo kupata alama ya ubora.
Akizungumza Juni 20, 2026, wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika jijini Dodoma, Masoy amesema kuwa wajasiriamali wengi hukumbana na changamoto katika mchakato wa uthibitishaji wa ubora kutokana na kuwasilisha bidhaa zao TBS bila kuwa na maandalizi na mafunzo ya kutosha.
Ameeleza kuwa SIDO hutoa mafunzo ya vitendo na darasani yanayolenga kuwajengea wajasiriamali ujuzi na maarifa ya kuzalisha bidhaa zinazokidhi viwango vinavyotakiwa vya ubora. Ameongeza kuwa bidhaa za kemikali, ikiwemo sabuni, zinahitaji uelewa wa kina wa masuala ya kemia ili kuhakikisha zinakidhi viwango vya usalama na ubora.
Aidha, Masoy amesema kuwa wajasiriamali wanaopata mafunzo kupitia SIDO hunufaika na fursa mbalimbali, ikiwemo kupata huduma za TBS bila gharama kwa kipindi cha miaka mitatu ya mwanzo. Amesisitiza umuhimu wa kutumia mafunzo hayo kama msingi wa kuzalisha bidhaa bora na zenye ushindani katika masoko ya ndani na kimataifa.









