Home Kitaifa DKT.JAFO ARIDHISHWA NA KASI YA MKANDARASI MRADI WA MAJI NYANI

DKT.JAFO ARIDHISHWA NA KASI YA MKANDARASI MRADI WA MAJI NYANI

Mbunge wa Jimbo la Kisarawe mkoani Pwani, Selemani Jafo, ameonesha kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi wa maji katika Kijiji cha Nyani, Kata ya Mafizi, akieleza kuwa hatua iliyofikiwa inaleta matumaini mapya kwa wananchi.

Mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya BROADWAYS ENGINEERING CO LTD una thamani ya shilingi milioni 402.8 na hadi sasa umefikia asilimia 70 ya utekelezaji, jambo linaloashiria kuwa upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa eneo hilo si wa muda mrefu tena.

Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji, mradi unahusisha ujenzi wa mnara wa tanki la maji lenye urefu wa mita 12 na uwezo wa kuhifadhi lita 50,000, pamoja na ujenzi wa vituo vitano vya kuchotea maji na ulazaji wa mtandao wa mabomba wenye urefu wa kilometa 16.167.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi huo, Dkt. Jafo alimpongeza mkandarasi kwa kufanya kazi kwa kasi na weledi mkubwa, akibainisha kuwa kampuni hiyo imeendelea na kazi hata kabla ya kupokea malipo yoyote, jambo alilolitaja kuwa ni uzalendo na kujitolea kwa maendeleo ya wananchi.

Kutokana na kasi hiyo, Jafo ameiiomba Wizara ya Maji kulipa kiasi cha shilingi milioni 279.1 kwa kazi zilizokamilika ili kumwezesha mkandarasi huyo kuendelea na hatua zilizobaki na kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.

Mbali na mkandarasi, mbunge huyo pia amempongeza Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kisarawe, Mhandisi Evangelista Kahwili, kwa usimamizi makini wa miradi ya maji ndani ya jimbo hilo, akisema nidhamu na ufuatiliaji wa karibu umechangia mafanikio yanayoonekana.

Wananchi wa Nyani na maeneo ya jirani wanatarajia kunufaika na mradi huo mara utakapokamilika, huku wakieleza kuwa utapunguza adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji na kuboresha afya pamoja na shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!