Home Kitaifa FCC YASEMA MAGEUZI YA SHERIA YATALINDA WALAJI, KUBANA BIDHAA BANDIA

FCC YASEMA MAGEUZI YA SHERIA YATALINDA WALAJI, KUBANA BIDHAA BANDIA

Tume ya Ushindani (FCC) imesema inaendelea na mageuzi ya sheria na mifumo yake ya kazi ili kuimarisha ushindani wa haki sokoni na kulinda walaji dhidi ya bidhaa zisizo na ubora.

Akizungumza February 24, 2026, katika semina ya tume hiyo na waandishi wa habari iliyofanyika kwenye Makao Makuu jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, amesema maboresho hayo yanalenga kudhibiti bidhaa bandia, kupambana na matangazo ya upotoshaji na kuhakikisha wafanyabiashara wanazingatia misingi ya ushindani wa haki.

Hata hivyo, ameongeza kuwa kuenea kwa bidhaa bandia kumeendelea kuwa changamoto kubwa inayohatarisha afya za wananchi, kupunguza mapato ya Serikali na kuwakosesha wafanyabiashara halali fursa ya kukuza biashara zao.

Jukumu letu ni kuhakikisha soko linakuwa salama na lenye ushindani wa haki. Hatuwezi kuruhusu bidhaa bandia kuharibu afya za wananchi na kuathiri uchumi wa nchi,” amesema Ngasongwa.

Hata hivyo, amebainisha kuwa FCC imejipanga kuongeza nguvu katika usimamizi wa soko kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali ili kuhakikisha bidhaa zinazoingia nchini zinakidhi viwango vinavyotakiwa.

Katika hatua nyingine, amesema tume inaendelea kushirikiana kupitia mtandao wa TANOGA ili kuimarisha uratibu kati ya taasisi za udhibiti na mawakala wa forodha.

Amesema matumizi ya mifumo ya kidijitali yataongezwa ili kupunguza mwingiliano wa moja kwa moja kati ya watumishi na wateja na hivyo kuongeza uwazi pamoja na kupunguza mianya ya vitendo visivyo vya kiadilifu.

FCC imesema itaendelea kutoa elimu kwa umma na kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha mazingira ya biashara nchini yanabaki kuwa shindani, salama na yenye manufaa kwa wananchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!