
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Mhe. Petro Magoti, amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya serikali kuacha uzembe na kufanya kazi kwa kuzingatia mikataba na viwango vilivyowekwa. Ameyasema hayo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la VETA lililopo Kata ya Kazimzumbwi, Tarafa ya Sungwi
Mhe. Magoti amesema jengo hilo lilitakiwa kukamilika mwaka 2023 ili wanafunzi waanze masomo mwaka 2024, lakini hadi sasa ujenzi wake unaendelea kusuasua, hali ambayo imekwamisha utekelezaji wa malengo ya serikali ya kuwawezesha vijana kupata elimu ya ufundi stadi kwa wakati.

Aidha, amewataka wakandarasi kuhakikisha wanaharakisha kazi kwa uwajibikaji, huku akisisitiza umuhimu wa kununua vifaa vya ujenzi katika maeneo ya karibu na mradi badala ya kuvifuata mikoa ya mbali, ilhali viwanda na wasambazaji vipo ndani ya Wilaya ya Kisarawe. Ameeleza kuwa hatua hiyo itapunguza gharama zisizo za lazima na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa mradi.
Mwisho, amesema serikali imeendelea kuchukua hatua kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati, na kwa sasa jitihada zinaendelea kufanyika huku akisisitiza usimamizi wa karibu wa wahandisi na matumizi sahihi ya fedha za umma ili jengo hilo likamilike na kuanza kutoa huduma kwa jamii kama ilivyokusudiwa.








