Home Kitaifa KUELEKEA MWAKA MPYA 2026, REA YAWASHIKA MKONO WAHITAJI

KUELEKEA MWAKA MPYA 2026, REA YAWASHIKA MKONO WAHITAJI

Kuelekea maadhimisho ya Mwaka Mpya 2026, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeendelea kugusa maisha ya Watanzania wenye mahitaji maalum kwa kutoa msaada wa kijamii na kuwapatia salamu za heri ya mwaka mpya ujao.

Zoezi la utoaji wa msaada kwa walemavu wa ukoma limeongozwa na Bi. Judith Abdalah kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy. Katika zoezi hilo, REA ilikabidhi mahitaji mbalimbali kwa Kikundi cha Walemavu wa Ukoma kilichopo Kata ya Hombolo, jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Bi. Abdalah aliwasilisha salamu za REA na kuwataka walemavu wa ukoma kuendelea kuishi kwa upendo, mshikamano na amani. Alisisitiza kuwa REA itaendelea kuwashika mkono kwa kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali ili kuwawezesha kukua kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi Tawi la REA (TUGHE), Bw. Swalehe Kibwana, alisema zoezi la kuwafikia na kuwasaidia wahitaji ni endelevu, na akaeleza kuwa REA itaendelea kutoa msaada hususan kwa walemavu wa ukoma waliopo Hombolo.

Naye Mwenyekiti wa Kikundi cha Wanawake na Samia Mkoa wa Dodoma, Bi. Fatuma Madudu, aliishukuru REA kwa kujitokeza kuwasaidia walemavu wa ukoma kwa kuwapatia mahitaji muhimu, akibainisha kuwa msaada huo una mchango mkubwa katika kuboresha maisha yao.

Aidha, Katibu wa Walemavu Hombolo alitoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kuwashika mkono walemavu wa ukoma kwa kuwapatia mahitaji muhimu ikiwemo chakula, ili nao waweze kufurahia kikamilifu sikukuu za kuukaribisha Mwaka Mpya 2026.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!