
Serikali imewataka wataalam wa ununuzi na ugavi nchini kuongeza ubunifu, uongozi bora na matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuongeza ufanisi, uwazi na tija katika matumizi ya fedha za umma. Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb).
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 16 la Wataalam wa Ununuzi na Ugavi lililoandaliwa na Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), jijini Arusha, Mhe. Mhandisi Munde alisema kongamano hilo lina kaulimbiu ya “Kukuza Wataalam wa Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi watakaojiimarisha katika Ujuzi wa Uongozi na Ubunifu”.
Alieleza kuwa Serikali imejipanga kuimarisha usimamizi wa manunuzi kupitia Mfumo wa Kidigitali wa Ununuzi wa Umma (NeST) kwa lengo la kupunguza gharama, kuongeza uwazi, kuharakisha utekelezaji wa miradi, kuzingatia bei ya soko na kuleta tija kwa Taifa.
“Serikali imeelekeza shughuli zote za ununuzi zifanyike kupitia Mfumo wa NeST ili kuongeza uwazi, kupunguza gharama na kuhakikisha thamani halisi ya fedha inapatikana katika miradi ya maendeleo,” alisema Mhe. Mhandisi Munde.

Aliongeza kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unategemea kwa kiasi kikubwa weledi na uadilifu wa wataalam wa ununuzi na ugavi. Hivyo, Serikali itahakikisha Sheria na Kanuni za Ununuzi wa Umma zinazingatiwa kikamilifu katika ngazi zote za Serikali na sekta binafsi.
Aidha, aliagiza PSPTB kushirikiana kwa karibu na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ili kuhakikisha shughuli zote za ununuzi na ugavi nchini zinafanywa na wataalam waliosajiliwa rasmi na PSPTB.
“Waajiri wote nchini wahakikishe wanawatumia wataalam waliosajiliwa na PSPTB kama inavyoelekezwa na Sheria Na. 23 ya Mwaka 2007 iliyoanzisha PSPTB. Hatua hii italeta weledi, uwajibikaji na kuepusha upotevu wa fedha za umma,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mhandisi Munde alisema kongamano hilo limewakutanisha wataalam, wakufunzi na wadau kutoka ndani na nje ya nchi kujadili namna ya kuimarisha ufanisi katika ununuzi na ugavi. Aliwataka washiriki kutumia fursa hiyo kupata maarifa mapya na kutoa mapendekezo yatakayoboresha sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa PSPTB, CSP. Jacob Kibona, alisema PSPTB imeendelea kusimamia na kukuza fani ya ununuzi na ugavi kwa kuhuisha mitaala ya mafunzo ya kitaaluma yenye kujikita katika umahiri, ili kuzalisha wataalam wenye ujuzi wa juu katika usimamizi wa mnyororo wa ugavi.

Aliongeza kuwa hatua hiyo inatekelezwa kupitia Miongozo ya Udhibiti wa Mitaala (Curriculum Accreditation Guidelines) inayolenga kulinda viwango vya taaluma na kuleta usawa kwa wahitimu wa fani hiyo katika vyuo vya umma na binafsi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, CPSP. Godfred Mbanyi, aliwapongeza washiriki wa kongamano hilo kwa mchango wao katika kuendeleza fani ya ununuzi na ugavi nchini. Alisisitiza kuwa PSPTB itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria ili kuhakikisha fani hiyo inaleta tija kwa Taifa na kusimamia vyema rasilimali za umma.






