Home Kitaifa WATANZANIA MILIONI 18 WANUFAIKA NA MFUKO WA UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI

WATANZANIA MILIONI 18 WANUFAIKA NA MFUKO WA UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI

Na Magrethy Katengu, Mzawa Media – Dar es Salaam

Serikali imeendelea kutekeleza jitihada za kuwawezesha wananchi kiuchumi, ambapo katika mwaka wa fedha 2024/2025 imetenga kiasi cha shilingi trilioni 2.44 kwa ajili ya mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, hatua iliyowezesha zaidi ya Watanzania milioni 18 kunufaika, wakiwemo wanaume asilimia 51 na wanawake asilimia 49.

Akizungumza Oktoba 10, 2025, wakati wa semina ya kuwajengea uwezo wanahabari kuhusu kazi na majukumu ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Kaimu Katibu Mtendaji wa NEEC, Bi. Neema Mwakatobe, alisema Baraza hilo linaendelea kufuatilia utekelezaji wa shughuli zote za uwezeshaji wananchi kiuchumi nchini.

Bi. Mwakatobe alisema kuwa NEEC ipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na jukumu lake kuu ni kuratibu, kufuatilia na kutathmini shughuli zote zinazotekelezwa na taasisi mbalimbali za uwezeshaji, ikiwemo TASAF, Halmashauri za Serikali za Mitaa, na taasisi nyingine za kifedha.

Alifafanua kuwa Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ilianzishwa mwaka 2004, ikifuatiwa na Sheria ya mwaka 2005 iliyounda rasmi Baraza hilo kwa lengo la kuhakikisha Watanzania wanashiriki ipasavyo katika uchumi wa nchi.

NEEC inafanya kazi kwa karibu na wizara, taasisi na wadau wa maendeleo wanaotekeleza programu za kuwawezesha wananchi. Tunahakikisha mipango hiyo inawafikia walengwa ili kuwaondoa kwenye umasikini kwa kuwapatia mikopo na dhamana,” alisema Bi. Mwakatobe.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari (JOWUTA), Bw. Selemani Msuya, aliishukuru NEEC kwa kuandaa semina hiyo na kutoa elimu muhimu kwa wanahabari.

Tunaishukuru NEEC kwa kutambua mchango wa waandishi wa habari. Kupitia semina hii, wanachama wetu watakuwa mabalozi wazuri wa kufikisha taarifa za uwezeshaji kwa wananchi,” alisema Bw. Msuya.

Aliongeza kuwa JOWUTA ina wanachama zaidi ya 500 nchi nzima, wakiwemo zaidi ya 150 kutoka mkoa wa Dar es Salaam, na akaomba NEEC kuendelea kutoa mafunzo kama hayo kwa waandishi wa habari wa mikoa mingine ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu fursa za kiuchumi.

Kupitia ushirikiano huo mpya kati ya NEEC na vyombo vya habari, inatarajiwa kuwa wananchi wengi zaidi watapata maarifa sahihi kuhusu fursa za kiuchumi, jambo litakaloongeza ushiriki wao katika shughuli za uzalishaji na kukuza uchumi wa Taifa kwa ujumla.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!