Home Kitaifa DKT. JAFO AWAHIDI WANANCHI UMEME, ELIMU, AFYA NA AJIRA

DKT. JAFO AWAHIDI WANANCHI UMEME, ELIMU, AFYA NA AJIRA

Mgombea ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Kisarawe, Dkt. Seleman Jafo, ameahidi kuendeleza kasi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo umeme, elimu, barabara, afya na ajira.

Akizungumza leo Septemba 11, 2025 katika kata ya Maneromango wilayani Kisarawe, Dkt. Jafo amesema kipaumbele chake ni kuhakikisha vitongoji vyote ambavyo bado havijapata huduma ya umeme vinapatiwa nishati hiyo ndani ya miaka mitano ijayo.

Katika sekta ya elimu, amesema tayari ameimarisha sekondari zilizopo kwa kujenga madarasa, mabwalo, mabweni na majengo ya utawala, huku sekondari za kidato cha tano na sita zikiongezeka kutoka moja ya awali hadi kufikia shule sita. Aidha, shule za msingi pia zimeimarishwa. Ameeleza kuwa hatua hizi zimefanikishwa kwa msaada mkubwa wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wa barabara, amesema ujenzi wa barabara kutoka kiwanda cha saruji hadi Sumbwi umekamilika, na kwamba Rais Samia tayari ametoa kibali cha kujengwa kwa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 34.5 kutoka Sumbwi hadi Msanga Chale, ambapo kinachosubiriwa sasa ni kusainiwa kwa mkataba ili ujenzi uanze.

Sekta ya afya nayo imepewa kipaumbele, ambapo vituo saba vya afya kwa sasa vinatoa huduma za upasuaji, huku vituo vingine viwili vikiwa vinaongezwa. Amesisitiza mpango wa kuhakikisha kila kata inakuwa na zahanati, akisema: “Kwa kampeni yangu, kila mtu atibiwe kwao. Hii kazi si ya mbunge pekee, bali ya kushirikiana na wananchi. Ndani ya miaka mitano tunahakikisha agenda ya zahanati inakamilika.”

Aidha, ameahidi kuanzisha viwanda vidogo na vya kati ili kufanikisha ajira kwa vijana wa Kisarawe, akibainisha kuwa ajira ni miongoni mwa changamoto zinazohitaji ufumbuzi wa haraka.

Mwisho, Dkt. Jafo amewaomba wananchi wa Kisarawe kumpigia kura ya ndiyo yeye pamoja na madiwani wa CCM, na pia amemwombea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kura za ndiyo, akisisitiza kuwa mshikamano huo ndio utakaohakikisha Kisarawe na Taifa kwa ujumla vinaendelea kupiga hatua kubwa za maendeleo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!