
Na Shomari Binda-Musoma
WANANCHI katika manispaa ya Musoma wamemtuma Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exauds Kigahe kufikisha salamu zao kwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuifungua kwa ufufuaji na ujenzi wa viwanda.
Salamu hizo wamezituma kwa Rais kupitia kikao cha wafanyabiashara wa manispaa ya Musoma na Naibu Waziri huyo kilicjofanyika leo februari 26 kwenye ukumbi wa uwekezaji uliopo ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mara.
Wakizungumza kwenye kikao hicho wamesema mji wa Musoma upo chini kiuchumi kutokana na kufa kwa viwanda vilivyokuwepo na kushindwa kuanzishwa kwa viwanda vipya.
Afidh Waziri mmoja wa wachangiaji kwenye kikao hicho amesema kama kutafunguliwa kwa viwanda vilivyokufa na kuanzishwa mji na mkoa wa Mara kiujumla utafunguka.
Amesema viwanda vipya vinaweza kuanzishwa kwa kupatikana kwa wawekezaji wageni watakaoshirikiana na wazawa wenye maeneo bila kuwepo kwa vikwazo.
” Tunashukuru umetuletea salamu za mheshimiwa Dkt.Samia na sisi tufikishie salamu zetu kwake kuwa tuna uhitaji wa viwanda Musoma na mkoa wa Mara kiujumla”,amesema.
Mmoja wa wafanyabiashara aliyewahi kumiliki kiwanda cha samaki cha Fishpark kilichokufa Gidion Mazara amesema zipo sababu zilizopelekea viwanda vya samaki kufa ikiwemo uvuvi haramu uliopelekea kupungua kwa samaki.
Amesema vipo vikwazo ambavyo kwa upande wake vimemkwamisha na kushindwa kuendeleza kiwanda cha maxiwa na hata kupelekea wawekezaji kuondoka.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi ( CCM) Wilaya ya Musoma mjini Benedict Magiri amesema kama viwanda vilivyokufa vitafufuliwa na kuanzishwa kwa viwanda vipya mji wa Musoma utainuka kiuchumi na kuwanufaisha wananchi.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka amesema serikali ya Dkt.Samia Suluhu Hassan itaendelea kufanyia kazi hoja za wananchi na kwa Musoma soko na stendi za kimkakati zimetolewa kibali cha kujengwa na kuuinua mji wa Musoma.
Akijibu maswali ya wananchi waliouliza kwenye kikao hicho,Naibu Waziri wa Viwanda Exaud Kigahe amesema serikali ina nia ya dhati kuwafikia wananchi kwenye maeneo na kusikiliza changamoto na kero zao ili kuweza kuzifanyia kazi.
Amesema yote yaliyozungumzwa na wananchi wa manispaa ya Musoma na mkoa wa Mara yanakwenda kufanyiwa kazi na serikali kwa sekta binafsi haipendi kuona mfanyabiashara anaanguka.
Naibu Waziri huyo amesema suala la viwanda amepita na amejionea mwenyewe kwa macho anakwenda kuliwasilisha ili serikali iweze kulifanyia kazi.
Amesema lengo la serikali ni kupatikana kwa Mali ghafi itakayopatikana ili kuweza kuwezesha viwanda vilivyokufa kufanya kazi na hoja ya kuvifufua inafanyiwa kazi.
” Nimekuwa nikipata msukumo mkubwa kutoka kwa mbunge wa jimbo la Musoma mjini Vedastus Mathayo kufika kujionea na nimefika nimeona tunakwenda kuja na majibu”amesema.
Kabla ya kuzungumza na wafanyabiashara hao wa manispaa ya Musoma Naibu Waziri huyo ametembelea viwanda vilivyokuwepo na kufa.
