
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Moremi Marwa, amesema uzinduzi wa Kituo cha Kijitonyama cha FTTX Experience Center ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa miaka 10 wa shirika hilo unaolenga kuboresha huduma kwa wateja na kuongeza ufanisi wa bidhaa zake.
Akizungumza leo Aprili 15, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi huo, Marwa amesema kituo hicho ni mojawapo ya hatua muhimu katika kufikia malengo ya awamu ya kwanza ya mpango mkakati huo, ambapo kipaumbele kikubwa kimewekwa katika kuboresha huduma kwa wateja na kuhakikisha wanapata huduma bora kwa urahisi zaidi.

“Kupitia kituo hicho, TTCL inalenga kusogeza huduma zake karibu zaidi na wateja, ikiwemo huduma za intaneti ya nyuzi (fiber) majumbani, maofisini na katika maeneo ya wazi kama vile viwanja vya michezo, vituo vya usafiri na masoko,” amesema.
Amesema shirika hilo linaendelea kupanua wigo wa bidhaa na huduma zake kwa kubuni vifurushi (bundles) vyenye bei nafuu ili kuwafikia watumiaji wengi zaidi, sambamba na kuendana na mahitaji ya soko la mawasiliano linalobadilika kwa kasi.
Marwa amebainisha kuwa utekelezaji wa mikakati hiyo umeanza kuzaa matunda, ambapo katika mwaka wa fedha uliopita shirika hilo limeongeza mapato na kupata faida ya shilingi bilioni 22.9, akikanusha taarifa zilizodai kuwa TTCL imepata hasara.
Amesisitiza kuwa mafanikio hayo yanatokana na ubunifu na utekelezaji wa miradi mbalimbali, ikiwemo vituo vya uzoefu kwa wateja, na kuwataka Watanzania kuendelea kutumia huduma za TTCL ili kuchochea maendeleo ya sekta ya mawasiliano nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), David Nchimbi, amesema maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano yana mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya kila siku ya Watanzania, hususan katika matumizi ya intaneti yenye kasi kubwa.
Ameeleza kuwa uwekezaji katika miundombinu ya mawasiliano unalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na zenye kuaminika, zitakazorahisisha shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Ameongeza kuwa matumizi sahihi ya teknolojia, hususan intaneti ya kasi, yanaweza kuongeza tija katika familia na jamii kwa ujumla, huku akihimiza Watanzania kuitumia kwa manufaa chanya, ikiwemo elimu, biashara na mawasiliano yenye tija badala ya matumizi yasiyo na tija.








